Shambulio la RSF dhidi ya msafara wa misaada wa UN Kordofan Kusini, Sudan lauwa mtu 1 na kujeruhi 2
-
RSF washambulai msafara wa misaada wa UN huko Kordofan Kusini
Wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan wameshambulia msafara wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika jimbo la Kordofan Kusini, na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine wawili.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeeleza katika taarifa yake leo Alkhamisi kuwa msafara huo ulishambuliwa katika mji wa Dilling ukielekea Kadugli, makao makuu ya jimbo la Kordofan Kusini.
Kwa mujibu wa mtandao huo, mtu mmoja ameuawa na madereva wawili wa malori wamejeruhiwa katika shambulio hilo.
"Msafara huo ulikuwa umebeba misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha ya raia zaidi ya 5,000 wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu," imeeleza taarifa ya Mtandao wa Madaktari wa Sudan.
Kundi hilo limelaani vikali shambulio la leo la wanamgambo wa RSF na kulitaja kuwa sehemu ya mashambulizi mtawalia ya wanamgambo hao dhidi ya misafara ya kimataifa ya misaada ya kibinadamu na kuzuia kufikishwa misaada hiyo kwa raia.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan umesisitiza kuwa kushambulia misafara ya misaada ya kibinadamu na kuzuia shughuli za utoaji misaada kwa raia ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Mtandao huo wa Madaktari wa Sudan umeitaka jamii ya kimataifa, Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinadamu kuhakikisha kuwa misaada ya kibinadamu inawafikia raia kote nchini Sudan kwa njia salama, endelevu na bila vikwazo vyovyote.
Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa ulisema kuwa raia 1,100 waliuawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kote nchini Sudan kati ya mwezi Januari na Juni mwaka huu.