UN yaidhinisha ombi la Afrika la kuichora tena ramani ya dunia, Marekani yapinga
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Ijumaa ya Septemba 04 limeidhinisha azimio la kura 164 za ndio na 1 ya hapana, linalolenga kurekebisha namna mabara yanavyoonekana kwenye ramani. Marekani ndiyo nchi pekee iliyopiga kura kulipinga azimio hilo.
Mfumo wa ramani unaotumika kwa kiasi kikubwa duniani ulianzishwa katika karne ya 16. Hata hivyo, una upotoshaji unaofanya maeneo ya nchi yaliyo mbali na Ikweta kuonekana makubwa zaidi, huku maeneo kama Afrika, Amerika ya Kusini na Asia ya Kusini yakionekana kuwa madogo kuliko ukubwa wake halisi.
Pendekezo hilo, lililopata kura 164 za kuunga mkono, linategemea takwimu za kisayansi na linalenga pia kurekebisha mitazamo ya kihistoria.
Pendekezo hilo linaloitwa “Rekebisha ramani”, linalenga kubadilisha uwakilishi wa kijiografia wa dunia ili kuonyesha kwa usawa zaidi ukubwa wa maeneo mbalimbali duniani.
Azimio hilo linaeleza kuwa ‘Mercator projection’, iliyobuniwa katika karne ya 16 kwa madhumuni ya urambazaji (hasa baharini), bado inatumika kwa kiasi kikubwa katika nyenzo za elimu, vyombo vya habari, mifumo ya kidijitali na nyaraka rasmi.
Mercator projection ni mfumo wa ramani wa silinda unaohifadhi umbo na pembe ambao uliwasilishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1569 na mwanajiografia na mtengeneza ramani kutoka Flanders, Gerardus Mercator.
Hata hivyo, mfumo huo una upotoshaji unaofanya maeneo ya kaskazini na kusini mwa Ikweta yaonekane makubwa zaidi, na kuifanya Afrika, Amerika ya Kusini na Asia ya Kusini kuonekana kuwa na ukubwa mdogo ikilinganishwa na ukubwa wake halisi.
Kwa mujibu wa azimio hilo lililoidhinishwa na Baraza Kuu, hali hiyo “inaendeleza mtazamo usio na uwiano kuhusu dunia.”
Azimio hilo linasema kurekebisha upotoshaji wa ukubwa wa mabara kwenye ramani ni hatua ya “haki ya kiakili na fidia ya kumbukumbu”, inayolenga kukuza uelewa wa pamoja miongoni mwa watu duniani.
Umoja wa Afrika umepitisha mfumo wa “Equal Earth” au ‘Dunia Sawa’, ambao ni aina ya ramani inayowakilisha kwa usahihi zaidi ukubwa wa mabara yote, hususan Afrika.
Kupitishwa kwa azimio hilo kunahimiza serikali, mashirika ya kimataifa na taasisi nyingine kutumia “Equal Earth”, ili kukuza uwakilishi unaoendana zaidi na ukubwa halisi wa maeneo mbalimbali ya dunia.
Akizungumza kabla ya kura, Waziri wa Mambo ya Nje wa Togo,
Azimio hilo, linaloungwa mkono na Muungano wa Afrika, linazitaja ramani kuwa nyenzo muhimu za elimu, sayansi na utamaduni, ambazo “huunda namna dunia inavyoonekana na taswira ya pamoja ya watu.”