Polisi Kenya yawaonya wanasiasa, yataka notisi za mikutano, maandamano zitolewe siku 3 kabla
-
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Polisi ya Kitaifa Kenya Muchiri Nyaga
Jeshi la Polisi la Kenya (NPS) limewaonya viongozi wa kisiasa na wafuasi wao kwamba litatekeleza kikamilifu Sheria ya Utulivu wa Umma wakati nchi hiyo inaingia katika kipindi cha kampeni za uchaguzi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, polisi ilisema imebaini visa vya kutovumiliana kisiasa, vurugu na uhalifu katika maeneo mbalimbali nchini.
NPS imesisitiza kuwa, yeyote anayepanga kufanya mkutano wa hadhara au maandamano lazima amjulishe mkuu wa polisi anayesimamia eneo husika kwa uchache siku tatu kabla, na si zaidi ya siku 14 kabla ya tukio hilo.
Taarifa hiyo ya kutoa notisi lazima ijumuishe maelezo ya mratibu, ukumbi au njia ya maandamano, tarehe na muda. Aidha, mikutano ya hadhara na maandamano sharti yafanyike kati ya saa kumi na mbili asubuhi na saa kumi na mbili jioni.
Taarifa hiyo iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Polisi ya Kitaifa Muchiri Nyaga, imesema taratibu hizo zitaiwezesha polisi kupanga vyema ulinzi na kuzuia makundi pinzani ya kisiasa kufanya matukio yanayokinzana katika eneo moja.
"Ni muhimu kutambua kuwa kutoa taarifa na kupata uthibitisho kuhusu mikutano yote inayokusudiwa kufanywa na wadau wa pande zote za kisiasa kwa afisa aliyeidhinishwa, ni hatua sahihi na halali inayoiwezesha polisi kutoa ulinzi madhubuti na wenye kuzingatia taarifa sahihi", imeeleza taarifa hiyo ya polisi.
Onyo hilo limetolewa wakati hekaheka za kisiasa zinaendelea kupamba moto kabla ya uchaguzi mkuu wa Kenya wa mwaka 2027, huku polisi wakitahadharisha kuwa vurugu, uchochezi na kuvuruga mikusanyiko halali havitavumiliwa.
Polisi ya Kenya imetamka kinagaubaga kwamba, watu wanaohusika na vurugu, kufadhili magenge ya uhalifu, kuchochea wafuasi au kuvuruga mikusanyiko halali "watashughulikiwa kwa ukali na kwa mujibu wa sheria". Aidha, imesisitiza kwamba msimamo wake unahusu pande zote za kisiasa na kwamba jeshi hilo litaendelea kutojihusisha na siasa na kutopendelea upande wowote.
"NPS inasisitiza tena kwa dhati kwamba hakuna mtu, -bila kujali hadhi ya kijamii, mrengo wa kisiasa, au wadhifa wa umma-, aliye juu ya sheria," taarifa hiyo imeongeza…/