Uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha moto uliosababisha vifo vya watu 22 harusini, Kinshasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141246-uchunguzi_unaendelea_kubaini_chanzo_cha_moto_uliosababisha_vifo_vya_watu_22_harusini_kinshasa
Mamlaka husika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeanzisha uchunguzi kuhusu moto uliotokea kwenye sherehe ya harusi jijini Kinshasa na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 22.
(last modified 2026-09-06T11:32:47+00:00 )
Sep 06, 2026 11:29 UTC
  • Watu 22 waaga dunia baada ya moto kutokea harusini Lingwala, Kinshasa
    Watu 22 waaga dunia baada ya moto kutokea harusini Lingwala, Kinshasa

Mamlaka husika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimeanzisha uchunguzi kuhusu moto uliotokea kwenye sherehe ya harusi jijini Kinshasa na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 22.

Imeelezwa kuwa moto huo ulianza katika jengo moja huko Lingwala usiku wa juzi Ijumaa na kuendelea hadi mapema jana Jumamosi.

Inaripotiwa kuwa njia nyembamba za kuingia eneo hilo ziliziba huku watu wakijaribu kukimbia moto huo.

"Tumekagua eneo lililoathiriwa na moto na ni wazi kuwa kanuni za usalama hazizingatiwi," ameeleza Norbert Nzindula, Meya wa Manispaa ya Lingwala alipozungumza na waandishi wa habari, jana.

"Kama unavyoona watu walipata shida kufika mahali salama, kila mtu alikuwa katika hali ya taharuki. Hili ni jambo la kusikitisha, hivyo tutachukua hatua; na mamlaka husika zitatekeleza hatua mbalimbali katika maeneo mengine ya kufanyia hafla ndani ya eneo la mamlaka yangu na katika jiji na jimbo zima la Kinshasa," aliongeza kusema Meya wa Manispaa ya Lingwala.

Matukio makubwa ya moto yamekuwa jambo la kawaida kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu jijini Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambapo mara nyingi majengo hujengwa bila kuwepo huduma muhimu kama vile huduma za kuzima moto.

Vyombo vya habari vya Kongo vimeeleza kuwa hali huwa mbaya zaidi wakati wa msimu wa kiangazi; na tayari matukio kadhaa ya moto yametokea mwaka huu.