Msaada wa kigeni kwa RSF ndio sababu kuu ya kuendelea kwa vita nchini Sudan
-
Waasi wa RSF
Msaada wa nje kwa kundi la waasi la Rapid Support Forces (RSF) ndiyo sababu kuu ya kuendelea kwa vita vya muda mrefu na jinai nchini Sudan. Hayo yamedokezwa na mwanasheria mkuu wa nchi hiyo siku ya Jumatatu, akitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti za kukomesha hali hiyo.
Intisar Ahmed Abdelaal alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha ripoti kwenye mazungumzo shirikishi ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuhusu Sudan, kama sehemu ya kikao chake cha 63 mjini Geneva, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Sudan.
Abdelaal pia anaongoza Kamati ya Taifa ya Sudan ya Kuchunguza Uhalifu na Ukiukaji wa Sheria za Kitaifa na Kimataifa.
Amelitaka baraza hilo kulaani msaada huo kwa waasi wa RSF kuchukua “hatua thabiti” za kuukomesha. Pia alithibitisha tena msimamo wa Sudan wa kukataa mifumo ya nje inayopuuza juhudi za kitaifa na akasisitiza upingaji wake wa azimio lililoanzisha Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Kutafuta Ukweli nchini Sudan.
Siku ya Alhamisi, ujumbe wa kutafuta ukweli wa UN ulisema kuwa mitandao ya msaada wa nje inachangia kuchochea vita nchini Sudan.Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamepata ushahidi unaoonyesha kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ilifundisha na kugharamia mamluki kutoka Colombia, ambao walishiriki katika mzingo na mauaji ya raia katika eneo la Darfur mwezi Oktoba uliopita.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa wapiganaji hao, ambao ni kati ya 2,000, waliajiriwa na kampuni inayopatikana nchini UAE yenye uhusiano wa karibu na serikali. Walifundishwa katika vituo viwili vya kijeshi nchini humo kabla ya kusafirishwa kwa njia ya ndege kuelekea katika eneo la Darfur, upande wa magharibi mwa Sudan, ripoti hiyo ilibainisha.
Jeshi la Sudan na RSF wamekuwa wakipigana tangu Aprili 2023 katika mzozo uliosababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kuwakimbisha makazi yao takriban milioni 13, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa na ya kimataifa.