Mufti wa Tanzania awataka Waislamu wafunge siku 3 kuomba El Nino iwe ya rehma, isiwe ya adhabu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141336-mufti_wa_tanzania_awataka_waislamu_wafunge_siku_3_kuomba_el_nino_iwe_ya_rehma_isiwe_ya_adhabu
Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally, ametoa wito kwa Mashekhe na Waislamu kwa ujumla kufunga kwa siku tatu kuanzia leo Alkhamisi Septemba 10, 2026, huku akiwataka wamuombe Mwenyezi Mungu aliepushe taifa na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotabiriwa.
(last modified 2026-10-15T07:22:56+00:00 )
Sep 10, 2026 02:49 UTC
  • Mufti wa Tanzania awataka Waislamu wafunge siku 3 kuomba El Nino iwe ya rehma, isiwe ya adhabu

Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally, ametoa wito kwa Mashekhe na Waislamu kwa ujumla kufunga kwa siku tatu kuanzia leo Alkhamisi Septemba 10, 2026, huku akiwataka wamuombe Mwenyezi Mungu aliepushe taifa na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazotabiriwa.

Akizungumza kuhusu taarifa za Serikali kupitia Idara ya Hali ya Hewa, Mufti Mkuu amesema kuna matarajio ya kunyesha mvua kubwa za El Nino katika maeneo mbalimbali nchini, kwa sababu hiyo, ametoa wito kwa viongozi wa dini na Waislamu wote kushiriki katika ibada hiyo ya kufunga na kumuomba Mwenyezi Mungu aiepushe nchi na majanga.

“Kwa mujibu wa maelezo au taarifa ya Serikali kupitia Idara ya Hali ya Hewa, inatarajiwa kunyesha mvua kubwa ya El Nino kote nchini kwa kiwango kikubwa sana,” amesema Sheikh Abubakar.

Kutokana na hali hiyo, Mufti Mkuu wa Tanzania amewataka Mashekhe wa mikoa, wilaya na kata, Maimamu, viongozi wa taasisi za Kiislamu pamoja na Waislamu wote kwa ujumla kufunga siku tatu na kutumia siku hizo kumuomba Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala aondoe mabalaa na majanga yanayoweza kujitokeza.

“Nachukua fursa hii kuwataka Mashekhe wa mikoa, Mashekhe wa wilaya, Mashekhe wa kata, Maimamu, Mashekhe wa taasisi zote nchini, na Waislamu wote kwa jumla, tufunge siku tatu kwanza, na tumuombe Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Ta’ala katika hizo siku tatu atuondoshee mabalaa na majanga makubwa, na madhara yanayotarajiwa kutokana na mvua ya El Nino,” amesema.

Aidha, Mufti Mkuu amewataka Waislamu wamuombe Mwenyezi Mungu afanye mvua hizo kuwa mvua ya rehema na yenye manufaa kwa jamii, badala ya kuwa chanzo cha adhabu na maafa.

“Na tumuombe Mwenyezi Mungu aifanye kuwa mvua ya rahma, mvua nzuri, isiwe mvua ya adhabu. Na atuondoshee aina zote za majanga na mabalaa,” amesisitiza Sheikh Abubakar.

Amemalizia kwa kutilia mkazo umuhimu wa kufunga na kuomba dua kwa pamoja ili kuiombea Tanzania ilindwe na madhara yanayoweza kutokana na mvua hizo.

“Tufunge siku tatu, tumuombe Mwenyezi Mungu atuondoshee majanga yanayotarajiwa kutokana na madhara ya mvua ya El Nino”.../