Maimamu sita wa Nigeria watekiwa wakiwa njiani kwenda kuombea kuchaguliwa upya kwa Rais
-
Rais Bola Ahmad Tinubu wa Nigeria
Watu wenye silaha wamewateka nyara maimamu sita nchini Nigeria kaskazini mwa nchi hiyo, Polisi wametangaza leo Jumapili.
Polisi katika jimbo la kaskazini-mashariki la Zamfara walieleza kuwa, siku ya Jumamosi, “kikundi cha majambazi wenye silaha, wanaodaiwa kumiliki silaha za kisasa, waliotea njiani kando ya barabara ya Dakko–Damri na kulizuia gari lililokuwa limewabeba wahanga hao.”
Taarifa ya Polisi imeongeza kuwa: “Wahanga hao sita, wote wakiwa ni Maimamu, walikuwa safarini kuelekea Talata Mafara walipozingirwa na kutekwa na watu hao.". Tukio hilo lilitokea yapata saa tano na nusu asubuhi kwa saa za huko.
Vyombo vya habari nchini Nigeria vimeripoti kuwa Maimamu hao walikuwa wageni wa Seneta Abdul’aziz Abubakar Yari. Gavana huyo wa zamani wa jimbo la Zamfara, ambaye ni kiongozi mwandamizi katika chama tawala cha All Progressives Congress (APC), alikuwa akiandaa hafla ya kidini nyumbani kwake Talata Mafara kwa ajili ya kuomba dua maalum ya kufanikisha kuchaguliwa tena kwa Rais Bola Tinubu katika uchaguzi wa Januari.
Polisi wa Zamfara waliongeza: “Vikosi vya usalama vimeanzisha msako mkali katika msitu karibu na eneo hilo ili kuwapata na kuwaokoa wahanga hao, sambamba na kuwatia mbaroni wahalifu.”
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Nigeria, majambazi hao wamedai fidia ili kuwaachia Maimamu hao. Gazeti la Daily Trust la Nigeria linaripoti kuwa zaidi ya viongozi wa dini 2,900 walikuwa wamealikwa katika kikao hicho cha maombi huko Zamfara.