Viongozi wa upinzani Kenya wasema wana hofu ya kuenea machafuko ya kisiasa na kuhatarisha uchaguzi wa 2027
-
Baadhi ya vinara wa upinzani Kenya
Viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani nchini Kenya wameonya kuwa ghasia za kisiasa zinaweza kuenea na kuhatarisha uchaguzi mkuu wa 2027.
Viongozi hao wakiongozwa na vinara wa vyama vya Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, Democratic Party, Justin Muturi na mwenzao wa DAP-Kenya, Eugene Wamalwa, wamesema wana wasiwasi kuhusu hali ya usalama nchini wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
Viongozi hao wameashiria tukio la hivi majuzi lililojiri katika kaunti ya Embu ambapo Naibu Rais Kithure Kindiki alilazimika kukimbilia usalama wake wakati wa mkutano wa hadhara baada ya kuzuka ghasia. Wamesema tukio hilo limeibua masuali kuhusu usalama wa viongozi na Wakenya wa kawaida. Musyoka amewataka Wakenya kuombeana amani, huku akiikosoa idara ya usalama kwa kile alichokitaja kuwa ni kumdhulumu Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji kufuatia tukio hilo.
Kiongozi wa chama cha DAP-Kenya Eugene Wamalwa, yeye amesema, viongozi wa upinzani wameazimia kuendelea kutembelea maeneo mbalimbali nchini licha ya uhasama waliokumbana nao katika baadhi ya maeneo. Amefananisha kuingia kwao Garissa na kuingia kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) huko Kismayu, Somalia, akisema walikumbana na upinzani kutoka kwa makundi aliyodai yalikuwa yamehamasishwa dhidi yao.
Wamalwa amedai kwamba makundi yaliyowakabili yalikuwa yamehamasishwa na Serikali.
Naye Kiongozi wa Democratic Party, Justin Muturi amesema, mazingira ya kisiasa nchini Kenya yamezidi kuwa yenye vikwazo, akidai kuwa maafisa wa usalama walizunguka kanisa ambako viongozi wa upinzani walikuwa wameenda kuomba.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, kanisa linazingirwa na maafisa wa usalama wenye silaha kwa sababu viongozi wa upinzani wameenda kuomba,” ameeleza kiongozi huyo na kuitaka serikali ihakikishe usalama wa kutosha unapatikana kwa Wakenya wote na viongozi wa kisiasa wakati nchi hiyo inajiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027…/