Askari 50 wa Mali, wapiganaji watano wa Kirusi wauawa katika shambulio kubwa la wanamgambo
Shambulio kubwa la kijeshi lililofanywa wiki iliyopita dhidi ya kambi kuu ya jeshi nchini Mali liliua askari wasiopungua 50 na wapiganaji watano wa kundi la Russia la 'Africa Corps'. Hayo yameripotiwa leo Jumatatu kwa vyombo vya habari na vyanzo vya kiusalama na vya eneo la tukio.
Shambulio la siku ya Alkhamisi iliyopita dhidi ya kambi ya kijeshi ya Dioura, ambalo kundi la waasi la JNIM limetangaza kuhusika nalo, ni moja ya mashambulio mabaya zaidi kuwahi kufanywa dhidi ya jeshi la Mali tangu ulipoanza mzozo ambao umeikumba nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.
Baadhi ya vyanzo vimeripoti idadi kubwa zaidi ya vifo, ikikadiriwa kuwa kati ya askari 60 na 80 katika kambi hiyo iliyoko kwenye eneo la kati la Mopti.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya kiusalama na vya eneo hilo, makumi ya askari wa Mali walitekwa pia katika shambulio hilo.
"Idadi ya vifo ni kubwa. Bila kuhesabu majeruhi, naweza kusema kuwa tunaomboleza vifo vya zaidi ya askari wetu 50, wakiwemo wanachama watano wa 'Africa Corps'," ameeleza afisa mmoja aliyekuwepo eneo la tukio.
Chanzo kingine cha usalama huko Mopti kimeripoti "kuuawa zaidi ya askari 60 katika shambulio hilo, pamoja na kutekwa wengine wapatao 60 ". Wakati huo huo, afisa wa eneo hilo aliyezungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP amesema "askari wasiopungua 80 waliuawa na wengi walitekwa"…/