Historia yaandikwa: Kenya mwenyeji wa kwanza Afrika wa mashindano ya dunia ya riadha 2029
Mji mkuu wa Kenya Nairobi uumechaguliwa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Dunia ya Riadha ya mwaka 2029, baada ya kushinda ushindani kutoka miji ya London, Munich na Rome.
Kwa uamuzi huo, Kenya itakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuandaa Mashindano ya Dunia ya Riadha. Hiyo ni kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha, World Athletics. Mashindano ya Dunia ya Riadha ya mwaka 2031 yatafanyika mjini Munich, Ujerumani, Shirikisho la Kimataifa la Riadha, World Athletics, limetangaza baada ya kikao cha Baraza lake kilichofanyika Jumanne ya jana Septemba 15 mjini Budapest, Hungary.
“Tumebahatika kupokea zabuni nne bora za kuandaa mashindano ya mwaka 2029 na 2031, na haikuwa uamuzi rahisi kwa Baraza,” alisema Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha Sebastian Coe, katika mkutano na waandishi wa habari.
Mashindano ya mwaka 2027 tayari yamepewa Beijing, China, kuwa mwenyeji.
“Uamuzi wa Baraza letu wa leo unamaanisha kwamba katika matoleo matatu yajayo ya Mashindano ya Dunia ya Riadha, tutaweza kuyafanyika katika mabara ya Asia, Afrika na Ulaya,” aliongeza Coe, raia wa Uingereza.
“Kuyapeleka Mashindano yetu ya Dunia barani Afrika kwa mara ya kwanza kutakuwa tukio la kihistoria. Nairobi imewasilisha zabuni yenye mvuto mkubwa na iliyojaa hisia,” alisema Coe.
Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha aliongeza: “Ilikuwa muhimu kwa Mashindano ya Duniaya Riadha kufanyika barani Afrika wakati ambapo tungepata mwenyeji sahihi, zabuni bora na mazingira yanayofaa. “Nairobi imedhihirisha wazi kwamba huu ndio wakati muafaka wa kuharakisha maendeleo ya mchezo wetu nchini Kenya na barani Afrika kwa ujumla, na kuacha urithi wenye nguvu utakaohamasisha kizazi cha watu katika bara zima.”
Kenya ni miongoni mwa mataifa yanayoheshimika zaidi duniani katika mchezo wa riadha, hasa katika mbio za masafa marefu na ya kati. Wanariadha wake wamekuwa wakifanya vizuri katika Mashindano ya Dunia ya Riadha, Michezo ya Olimpiki, mbio za nyika na mashindano makubwa ya mbio za marathon. Mafanikio hayo yameifanya Kenya kuwa moja ya nguzo muhimu za riadha barani Afrika na duniani. Nchi hiyo imeendelea kuzalisha wanariadha mashuhuri na kushinda medali nyingi katika mashindano ya kimataifa.