IOM: Karibu Wasudan 100,000 wamekimbia makazi yao katika jimbo la Blue Nile
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141486-iom_karibu_wasudan_100_000_wamekimbia_makazi_yao_katika_jimbo_la_blue_nile
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, karibu Wasudan 100,000 wamekimbia makazi yao katika jimbo la Blue Nile, kutokana na kuongezeka ghasia na mapigano katika eneo hilo.
(last modified 2026-09-16T02:55:16+00:00 )
Sep 16, 2026 02:53 UTC
  • IOM: Karibu Wasudan 100,000 wamekimbia makazi yao katika jimbo la Blue Nile

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa, karibu Wasudan 100,000 wamekimbia makazi yao katika jimbo la Blue Nile, kutokana na kuongezeka ghasia na mapigano katika eneo hilo.

Gazeti la Middle East Monitor limelinukuu Shirika la Kimataifa la Uhamiaji likisema, takwimu za kipindi cha kuanzia Januari 11 hadi Agosti 23 zinaonyesha kuwa jumla ya watu 99,277, sawa na kaya 19,497, wamefurushwa kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo la Blue Nile nchini Sudan.

Takwimu hizo mpya zinaonyesha ongezeko la asilimia 66 la idadi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao, ikilinganishwa na takwimu za awali za shirika hilo zilizotolewa tarehe 21 Mei mwaka huu. Wakati huo, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji liliripoti kuwa watu 59,742 walikuwa wamekimbia makazi yao katika jimbo hilo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, karibu nusu ya watu waliokimbia makazi yao, sawa na asilimia 47, ni watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

Tangazo la Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limeeleza pia kuwa Wasudan waliolazimika kuyahama makazi yao wamehamia katika maeneo saba tofauti katika jimbo lote la Blue Nile.

Kwa mujibu wa shirika hilo, asilimia 58 ya watu hao wanaishi katika maeneo yasiyo rasmi ya makazi, huku asilimia 9 wakiwa wamepata hifadhi katika nyumba za familia zinazowakaribisha. Aidha, asilimia 33 ya waliokimbia makazi yao wamejisitiri katika shule na majengo mengine ya umma.

Jimbo la Blue Nile, lililoko kusini-mashariki mwa Sudan, katika siku za hivi karibuni limekuwa likishuhudia kuongezeka mapigano kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) pamoja na washirika wao wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Sudan – Kaskazini (SPLM-N) katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.