May 29, 2018 03:18 UTC
  • Sudan yatetea na kuhalalisha kushiriki kwake katika mauaji ya wananchi wa Yemen + Picha

Waziri wa Ulinzi wa Sudan Luteni Jenerali Awad Mohamed Ahmed Ibn Auf amesema, kwa mtazamo wa kimaadili ni wajibu kwa nchi hiyo kutuma wanajeshi wake Yemen ili kuusaidia utawala wa Aal Saud katika vita dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Ahmed bin Aouf ameyasema hayo mjini Khartoum katika mazungumzo na balozi wa Saudi Arabia nchini humo Jaafar bin Mualla.

Tangu mwaka 2015, Sudan imetuma idadi kadhaa ya askari wake nchini Yemen kwa tamaa ya kupatiwa msaada wa fedha na utawala wa Aal Saud. Hadi sasa idadi kubwa ya askari hao wameuawa katika uvamizi huo wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen.

Baadhi ya wanajeshi wa Sudan waliouawa nchini Yemen

Kwa miezi kadhaa sasa wananchi na baadhi ya shakhsia wa kisiasa nchini Sudan wamekuwa wakikosoa uamuzi huo uliochukuliwa na viongozi wa serikali yao na kutaka wanajeshi wa Sudan waondoke nchini Yemen.

Mwezi Machi mwaka 2015, na kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa, Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen sambamba na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa ardhini, angani na baharini. Moto wa vita uliowashwa na Saudia na waitifaki wake nchini Yemen, hadi sasa umeteketeza roho za Wayemeni zaidi ya 14,000, umewajeruhi makumi ya maelfu na kusababisha mamilioni ya wengine kubaki bila makazi.

Idadi nyingine ya wanajeshi wa Sudan waliouawa Yemen

 

Uvamizi wa kijeshi ulioanzishwa na utawala wa Aal Saud vilevile umeisababishia nchi hiyo masikini ya Kiarabu uhaba mkubwa wa chakula na dawa.

Hata hivyo kutokana na muqawama wa wananchi wa Yemen, Saudi Arabia na waitifaki wake hadi sasa wameshindwa kufikia malengo yao nchini humo ya kuwaweka madarakani vibaraka wao.../

Tags