Samia Suluhu achaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza mwanamke wa chama tawala Tanzania, CCM
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i69620-samia_suluhu_achaguliwa_kuwa_mwenyekiti_wa_kwanza_mwanamke_wa_chama_tawala_tanzania_ccm
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata kura zote 1,862, sawa na asilimia 100 ya kura zilizopigwa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM unaoendelea kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 30, 2021 10:46 UTC
  • Rais Samia Suluhu Hassan
    Rais Samia Suluhu Hassan

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata kura zote 1,862, sawa na asilimia 100 ya kura zilizopigwa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM unaoendelea kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Uzoefu wa miaka 34 wa kuwa Mwanachama wa CCM na tajiriba ya miaka 44 akiwa mtumishi wa Serikali vimetajwa kuwa miongozi mwa vigezo vilivyomfanya Bi Samia Suluhu kuwa mwanamke wa kwanza mwenye sifa na uwezo wa kukiongoza chama hicho tawala nchini Tanzania.

Vilevile uwezo wake aliouonesha wa kufanya kazi kama Makamu wa Rais chini ya rais wa zamani wa Tanzania, John Magufuli na hatimaye kuwa Rais wa Tanzania baada ya kifo cha Magufuli vimemfanya Samia Suluhu aaminiwe kwamba anatosha kuwa Mwenyekiti wa chama hicho kinachotawala nchi kwa miongo kadhaa sasa.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama cha CCM pia wamemchagua Daniel Chongolo kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama hicho. Chongolo ambaye amependekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua nafasi hiyo, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam.

Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM, Dodoma

Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM pia imemchagua aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho. Shaka anachukua nafasi inayoachwa na Humphrey Polepole ambao waliteuliwa kuwa mbunge.

Miongoni mwa mambo yaliyoshuhudiwa leo katika Mkutano Maalumu wa CCM mjini Dodoma ni kurejea wenyekiti wawili wa kanda wa Chadema katika chama cha CCM.

Chama Kikuu cha upinzani cha Chadema kimepata pigo kubwa kwa kuondokewa na wenyeviti hao wawili wa kanda ambao ni Lazaro Nyalandu wa Kanda ya Kati na Suleiman Mathew wa Kanda ya Kusini.

Nyalandu ametangaza uamuzi huo hii leo mbele ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano Mkuu Maalumu kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma.