Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan: Tunafanya juhudi za kufikia mapatano kuhusu Bwawa la Renaissance
-
Mariam al-Sadiq al-Mahdi
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Sudan amesema nchi yake ina azma kubwa ya kufikia mapatano madhubuti na nchi jirani ya Ethiopia kuhusiana na kadhia ya kujazwa maji na kuanza kufanya kazi bwawa hilo.
Mariam al-Sadiq al-Mahdi ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Rais Macky Sall wa Senegal mjini Dakar akimuomba kufanya jitihada za kuhakikisha mgogoro wa ujenzi wa Bwawa la Renaissance juu ya maji ya Mto Nile huko Ethiopia unatatuliwa kwa njia za amani.
Mariam al Mahdi amesema Khartuom ina matumaini ya kufikiwa mapatano yatakayokidhi mahitaji na maslahi ya pande zote tatu za Ethiopia, Misri na Sudan chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika na washirika wa kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Sudan pia amesema mipaka ya Sudan na Ethiopia unalindwa na makubaliano ya kimataifa na kwamba Khartuom inafanya jitihada za kuikinaisha Addis Ababa ili iheshimu makubaliano na sheria za kimataifa. Amesisitiza kuwa jeshi la Sudan linadhibiti maeneo yote ya ardhi ya nchi hiyo.
Wakati huo huo chama tawala nchini Ethiopia kimetangaza kuwa, zinafanyika juhudi za kutekeleza awamu ya pili ya kujaza maji katika Bwawa la Renaissance.
Taarifa ya chama hicho imesema "maadui wa Ethiopia" wanataka kuibua vita na nchi jirani kwa ajili ya kudhoofisha uchumi wa Ethiopia na ksitisha miradi yake ya maendeleo.
Tarehe 30 Machi mwaka huu Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri alisema kuwa, maji ya Mto Nile ni mstari mwekundu na kwamba hatua yoyote ya Ethiopia katika maji ya mto huo itafuatiwa na jibu kali litakalotishia usalama wa kanda hiyo mzima.
Addis Ababa inasisitiza kuwa awamu ya pili ya kujaza maji katika bwawa hilo itafanyika kwenye miezi ya Julai na Agosti hata bila ya maafikiano na nchi za Misri na Sudan ambazo zinapinga vikali suala hilo.
Nchi mbili za Misri na Sudan zina wasiwasi kwamba, ujenzi wa Bwawa la Renaissance juu ya maji ya Mto Nile utapunguza mgao wao wa maji na kusababisha tatizo kubwa la maji katika nchi hizo.