Sep 01, 2021 02:52 UTC
  • Maelfu ya watu wakumbwa na tatizo la kuhara baada ya maji ya mto kuchafuka, Kongo

Maafisa wa afya katikka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameripoti kuwa, maelfu ya watu wamepatwa na tatizo la kuhara katika jimbo la Kasai katikati mwa nchi hiyo baada ya raia kutumia maji machafu na samaki waliokufa kutoka katika ziwa ambalo maji yake yamechafuka.

Maafa hayo ya kibinadamu yameripotiwa baada ya eneo la uchimbaji wa almasi nchini Angola kuripotiwa kutoa mada za sumu tangu mwezi Julai mwaka huu ambazo zimechafua maji katika mito ya Kasai na Tshikapa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

Mto Kasai nchini Kongo ambao maji yamechafuka 

Eve Bazaiba Naibu Waziri Mkuu Anayeshugulikia Mazingira wa Angola amewaambia waandishi wa habari baada ya kulizuru eneo lililoathirika kwamba: Zaidi ya kesi 4000 za kuhara zimesajiliwa katika maeneo 13 kati ya 18 yaliyoathiriwa katika jimbo la Kasai. 

Maafisa wa serikali katika jimbo la Kasai wamesema kuwa, maji ya mto mkoani humo yalibadilika rangi na viboko na samaki waliokufa walikutwa kwenye maji hayo yaliyochafuka. Bazaiba ameongeza kuwa, wakazi wa maeneo athirika wametakiwa kujiepusha kula samaki waliokufa. 

Wasiwasi umetanda katika Mto Kongo ambao ni wa pili kwa urefu barani Afrika ukitanguliwa na Mto Nile kwamba nao pia unaweza kukumbwa na hali hiyo kutokana na Mto Kasai kuingiliana na mto huo. Wakati huo huo watafiti wa Kikongo huko Kinshasa wametahadharisha kuwa, maji yaliyochafuka huwenda yakawa na athari hasi kwa miaka kadhaa.

Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kasai wameeleza kuwa, wamepatwa na vijiupele mwilini baada ya kutumia maji hayo machafu. Tayari serikali ya Kinshasa imechukua hatua za kuhakikisha kuwa, maji safi yanapelekwa katika maeneo yaliyoathirika. 

Tags