Jan 30, 2023 03:10 UTC
  • Watu 15 wateketea kwa moto katika ajali ya barabarani nchini Nigeria

Watu 15 wameteketea kwa moto baada ya basi moja kugongana na lori, kusini magharibi mwa Nigeria.

Hayo yameripotiwa na shirika la habari Sputnik ambalo limeongeza kuwa, takriban watu 15 wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria kugongana na lori na kuwaka moto huko katika eneo la Odigbo la jimbo la Ondo, la kusini magharibi mwa Nigeria.

Ripoti hiyo imesema ajali hiyo ilitokea jana asubuhi na polisi pamoja na vikosi vya kutoa msaada vilipelekwa haraka kwenye eneo la ajali hiyo. 

Kwa upande wake shirika la habari la "Sahara Reporters" nalo limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, basi hilo liliwaka moto baada ya kugongana na lori hilo na kupelekea zaidi ya watu 15 kuteketea kwa moto.

Chanzo cha ajali hii ni dereva wa moja kati ya magari hayo mawili kutoka upande wake na kuingia upande wa pili wa barabara kwa sababu zisizojulikana.

Pamoja na hayo, hadi inaripotiwa habari hii, serikali ya Nigeria ilikuwa bado haijatoa tamko lolote kuhusiana na suala hili.