Jun 02, 2023 02:12 UTC
  • Wataalamu wa afya watoa indhari juu ya mzozo wa lishe mashariki mwa Afrika

Wataalamu wa afya ya lishe Mashariki mwa Afrika wametahadharisha kuwa, mzozo wa lishe ni hali halisi katika mataifa 10 eneo hilo na unahitaji kutafutiwa ufumbuzi wa dharura.

Wajumbe kutoka mataifa hayo wanakutana Uganda kubadilishana maarifa na uzoefu kuhusu jinsi ya kukabiliana na kiwango cha juu cha utapiamlo, njaa na pia magonjwa yanayohusiana na lishe isiyofaa.

Mzozo wa lishe unaelezewa na Shirika la Afya Duniani WHO pamoja na mamlaka ya maendeleo ya serikali za pembe ya Afrika IGAD kuwa tishio kwa maisha yao kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa usalama na bei ya juu ya vyakula.

Mzozo huu unatajwa kutishia ongezeko la utapia mlo katika mataifa ya pembe ya Afrika, bonde la mto Nile, pamoja na kanda ya maziwa makuu na hasa kwa watoto walio chini ya miaka mitano, mama zao pamoja na wakongwe wasioweza kujitafutia riziki ya kila siku.

Kulingana na takwimu ambazo zimekusanywa na mashirika mbalimbali ikiwemo lile la mpango wa chakula duniani WFP, viwango vya utapiamlo na njaa viko juu katika mataifa ya Ethiopia, Kenya na Somalia. Inaelezwa kuwa, hadi watu milioni kumi katika nchi hizo wanahitaji misaada ya lishe.

Ijapokuwa hali ya lishe ni afadhali katika mataifa mengine kwa ulinganisho, tatizo kubwa ni bei ya chakula ambayo imesababishwa na misukosuko ya kiuchumi duniani kutokana na vita na pia hali ya jamii nyingi kuendelea kutegemea tu misimu ya mvua.