Israel yatwangwa kwa zaidi ya makombora 50 katika kipindi cha dakika mbili + Video
(last modified Thu, 24 Oct 2024 11:55:18 GMT )
Oct 24, 2024 11:55 UTC
  • Israel yatwangwa kwa zaidi ya makombora 50 katika kipindi cha dakika mbili + Video

Jeshi la utawala wa Kizayuni limetangaza kuwa, maeneo ya al Jalil ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni yamepigwa kwa makombora 50 katika kipindi cha dakika mbili huku Israel ikishindwa kutungua makombora hayo.

Televisheni ya al Alam imetangaza habari hiyo leo Alkhamisi na kusema kuwa, zaidi ya makombora 50 yamevurumishwa kutokea Lebanon na kupiga maeneo ya al Khalil, kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina bandia la Israel na kwamba utawala wa Kizayuni umeweza kutungua baadhi tu ya makombora hayo.

Wakati huo huo redio ya utawala wa Kizayuni imenukuu matamshi ya afisa mmoja wa kijeshi wa Israel akikiri kwamba, kwa mara ya kwanza tangu vianze vita kati yao na Hizbullah, harakati hiyo ya mapambano ya Kiislamu imeyashambulia maeneo ya al Khalil kwa zaidi ya makombora 50 katika kipindi cha dakika mbili tu.

Chombo hicho cha habari cha Kizayuni kimekiri kwamba Wazayuni wanne wamejeruhiwa katika shambulio hilo. Tab'an utawala wa Kizayuni unachuja mno habari zinazohusiana na vipigo inavyopata kutoka kwa wanamapambano wa Kiislamu. Hakuna chombo chochote cha habari cha Israel kinachoruhusiwa kutangaza habari yoyote ile bila ya kupitia kwanza kwenye mchujo mkali wa jeshi la utawala wa Kizayuni.

 

Kabla ya hapo pia duru za Kizayuni zilikuwa zimetangaza kwamba, ving'ora vya hatari vimesikika mapema leo alfajiri vikilia mfululizo katika maeneo 17 tofauti ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni. Ving'ora hivyo vimelia kutokana na wimbi la makombora ya Hizbullah yaliyokuwa yanamiminika kwenye maeneo ya Wazayuni.