Kama si Iran, nani atakayeunusuru ulimwengu na shari ya wazi na iliyojificha ya Israel?
Kwa miaka mingi sasa Israel imekuwa ikitekeleza sera za ardhi iliyochomwa (scorched-earth policy) katika eneo la Asia Magharibi. Kuanzia mashambulizi yasiyosita katika Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari ya raia wa Palestina hadi kuwauwa kigaidi wasomi wa nyuklia wa Iran na mashambulizi ya anga dhidi ya Syria, ni sehemu ya sera za Israel ambazo zimejikita katika kueneza vita na hali ya mchafukoge.
Makala ya karibuni ya jarida la Newsweek iliyopewa jina "Israel Inaweza Kuunusuru Ulimwengu Mbele ya Iran ya Nyuklia" iliyoandikwa na Yaakov Katz, mtafiti wa ngazi ya juu katika taasisi ya Kiyahudi ya Jewish People Policy, kama zilivyokuwa bwabwaja nyingine za jarida hili linalochochea vita la Marekani, kinyume chake inaonekana kuwa makala hiyo isiyo na mantiki imeandikwa kwa ajili ya kuchochea vita na propaganda za taasisi za kijeshi na kiuchumi zinazounga mkono vita. Katika makala hii, mwandishi ambaye ameonekana kujiamini kupindukia na kutumia mbinu ya kujenga usahaulifu wa muda katika akili ya hadhira kuhusu jinai zinazoendelea kufanywa na Israel, amedai kuwa Israel iko tayari peke yake kuuokoa ulimwengu wa kikoloni wa Magharibi na tishio la Iran. Hata hivyo swali kuu linaloulizwa hapa ni kuwa, kama Iran isingekuwepo, nani atakayekabiliana na shari kuu zaidi yaani Israel? Nani atasimama kupambana na upenyaji wa wazi na wa siri wa Uzayuni ambao umevuruga siasa za kimataifa na kuifanya sehemu moja ya eneo la Asia Magharibi kuwa ardhi iliyoteketezwa kwa moto?
Israel, utawala unaovuruga siasa za dunia kwa hatua zake za kujitanua
Nafasi ya Israel katika kuibua migogoro mingi duniani kwa njia ya moja kwa moja na kinyume chake, haiwezi kupingwa. Ushawishi wa taasisi za Kizayuni katika siasa za kimataifa hususan huko Marekani, Ulaya na hata katika Umoja wa Mataifa umeziondoa sera za dunia katika mkondo wa uadilifu na amani. Kuanzia makundi ya lobi zenye nguvu kama vile AIPAC ambayo yanatumia sera ya mambo ya nje ya Marekani kwa ajili ya kuhudumia maslahi ya Israel, hadi juhudi za kutaka kuvuruga makubaliano ya amani; yote hayo yanaonyesha nguvu haribifu za Israel katika upeo wa dunia.
Kwa mfano tu, katika miongo kadhaa iliyopita, Israel imejaribu mara kwa mara kuzishawishi serikali za nchi za Magharibi kuzuia kuundwa muungano au kufikiwa makubaliano yoyote ambayo yangeyanufaisha mataifa ya Asia Magharibi. Kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Iraq mwaka 2003 kwa kutegemea taarifa za uongo kwamba nchi hiyo ilikuwa na "silaha za maangamizi ya halaiki" kuliambatana na uungaji mkono wa moja kwa moja wa lobi za Kizayuni; na matokeo yake ni kuharibiwa Iraq na kuanzishwa makundi ya kigaidi kama vile Daesh yaani ISIS.
Mauaji ya wazi na kuenea vita Asia Magharibi
Kama tulivyosema mwanzoni mwa kipindi, Israel inatekeleza sera ya "ardhi iliyochomwa" (scorched-earth policy) katika Asia Magharibi kwa miaka kadhaa sasa. Kuanzia mashambulizi yasiyosita katika Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari ya raia wa Palestina hadi kuwauwa kigaidi wasomi wa nyuklia wa Iran na mashambulizi ya anga dhidi ya Syria, ni sehemu ya sera za Israel ambazo zimejikita katika kueneza vita na hali ya mchafukoge.
Ukanda wa Gaza, ambao ni jela ya wazi yenye watu milioni 2, ni nembo ya sera za kikatili za utawala wa Israel. Mashambulizi ya kila uchao katika eneo hilo na kuzishinikiza nchi za Magharibi kuwawekea vikwazo vya kikatili watu wa ukanda huo, ni sehemu tu ya ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu unaofanywa na Israel. Hata hivyo, dunia imekaa kimya kutokana na ushawishi mkubwa wa Israel katika taasisi za kimataifa.
Kuvuruga demokrasia na kueneza ugaidi
Kipengele kingine cha uharibifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ni juhudi zake za kuendelea kudhoofisha demokrasia katika nchi za kanda hii na hata katika maeneo mengine duniani. Huko Misri, Israel iliunga mkono mapinduzi ya kijeshi ya Abdel Fattah al-Sisi na kuchochea kukandamizwa harakati za wananchi. Nchini Iran, Israel imefanya kila inaloweza kuibua machafuko na kudhoofisha mamlaka ya uongozi wa nchi kwa kuyaunga mkono na kuyasaidia makundi ya kigaidi kama kundi la kigaidi la MKO na kutekeleza oparesheni za uharibifu.
Nje ya eneo la Magharibi mwa Asia, Israel imehusika katika mauaji ya kigaidi na kujipenyeza katika nchi za Ulaya na kadhalika. Kuanzia faili la majasusi wa Mossad nchini Ujerumani, jaribio la kuingilia uchaguzi wa Uingereza, kuvuruga uhusiano wa India na Pakistani kupitia uharibifu wa hujuma za mtandao na kueneza habari za uwongo, mchango wake katika kuigawa Sudan, kutumia sehemu ya uhusiano wa kigeni wa Argentina kwa maslahi yake, kutwisha matakwa yake katika uhusiano wa kigeni wa Poland, ushawishi wake katika mabunge ya Ufaransa na Hungary, mkono wake katika kuharibu uhusiano kati ya Morocco na Uhispania kama ilivyothiibitishwa na data ya Facebook, mkono wake katika kuchochea mivutano ya kikabila nchini Libya na ujasusi na utekaji nyara wa watu huko Kusini-Mashariki mwa Asia kama vile Indonesia na Thailand, yote haya yanaonyesha kuwa hatua za Israel ni tishio kwa demokrasia ya kimataifa.
Kugeuza Asia Magharibi kuwa ardhi iliyotekelezwa (scorched-earth)
Lengo kuu la siasa za kivita za Israel ni kuanzisha eneo dhaifu, lenye migawanyiko na lisilo na utulivu ambalo halina nguvu ya kukabiliana na utawala huo. Kwa kuanzisha na kuunga mkono vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Syria, Yemen na hata Iraq (hasa kupitia kampeni yake ya mauaji ya wanasayansi), Israel imegeuza sehemu ya ardhi hii kuwa sehemu ya magofu ambako hakuna nguvu inayoweza kuwa tishio kwa utawala huo.
Udanganyifu wa Nguvu za Kijeshi za Israel: Ngumi Zinazopiga Upepo
Makala ya Newsweek inajaribu kuidhihirisha Israel kama nguvu kubwa ya kijeshi isiyoweza kushindwa. Lakini ukweli ni kwamba, nguvu ya kijeshi ya Israel, ingawa imenufaika na teknolojia ya kisasa ya Marekani, imeonyesha udhaifu na fedheha yake dhidi ya Hizbullah ya Lebanon, Iran, na hata Hamas, na imeweza tu kujitutumua dhidi ya zana zilizodumaa za Syria. Katika miezi ya hivi karibuni, Iran imefanya mara mbili mashambulizi ya makombora dhidi ya utawala wa Israel kwa operesheni zilizopewa jina la "Ahadi ya Kweli", (Operation True Promise) ambayo sio tu yalitoa changamoto kubwa na kuharibu baadhi ya mifumo ya ulinzi ya Israel, lakini pia yalilenga nukta na vituo muhimu vya kimkakati vya utawala huo. Katika operesheni ya pili ya Iran, kama ilivyothibitishwa na video zilizosambazwa katika vyombo vya habari, zaidi ya 70% ya makombora yaliyoonekana yalivuka salama mifumo ya ulinzi ya Israel na kulenga shabaha zilizokusudiwa. Takwimu za Iran zinaonyesha kuwa, makombora zaidi ya 180 kati ya 200 yaliyotumiwa katika Operation True Promise yalipiga shabaha kwa umakini mkubwa. Kwa upande mwingine, Hizbullah ya Lebanon, mbali na kuuawa shahidi idadi kadhaa ya makamanda wake akiwemo katibu mkuu wake mashuhuri, bado iko hai kama jeshi lenye nguvu la Mhimili wa Muqawama, na hata kasi ya kujisasisha na kutibu majeraha ya harakati hiyo imewashangaza watu wote. Katika vita vya hivi majuzi, licha ya nguvu zake zote za kijeshi za Marekani, Israel haikuweza kuifuta Hizbullah kwenye mlingano wa nguvu na imelazimika kukubali usitishaji wa mapigano ambayo kivitendo unaiweka Hizbullah katika nafasi inayokubalika.
Wakati huo huo, Hamas inaendelea kutoa vipigo vikubwa kwa Israel, licha ya madai ya mwandishi wa wa Newsweek kwamba harakatii hiyo "imeangamizwa kikamilifu." Mashambulizi ya mara kwa mara ya Hamas dhidi ya vituo na magari ya kivita ya Israel na hata mauaji ya askari wa utawala huo ghasibu wanaoua watoto, yanaonesha kuwa, harakati hiyo haijaangamizwa, bali limekuwa kikosi cha mapambano kisichotabirika kwa kufuata stratijia ya vita vya mwituni. Jambo muhimu zaidi kuhusu Hizbullah na Hamas nii kwamba, kama inavyothibitishwa na historia, mara zote hupata nguvu na kuwa ngangari zaidi ya hapo awali, kwa hiyo Israel inapaswa kutarajia nyakati ngumu zaidi katikka siku za usoni.
Vita kwa Ajili ya Faida: Uchumi wa vita nyuma ya pazia la uchambuzi wa Newsweek
Makala ya Yaakov Katz katika jarida la Newsweek ni kama ndoto ya usingizini na mawazo ya mchezo wa vita ya kitoto kuliko uchanganuzi wa kweli na wa kimantiki. Badala ya kuwasilisha mtazamo wa kina kuhusu hali hali halisi ya Asia Magharibi, mwandishi anataka kuthibitisha mawazo yake ya kuchochea joto.
Kinachoonekana waziwazi katika makala ya Newsweek ni kwamba kutetea vita na Iran ni mradi wenye faida kwa makampuni ya silaha na lobi za kijeshi. Kwa sababu, vita, mwishowe, havina faida yoyote isipokuwa kwa tasnia ya kijeshi ya Magharibi ya kikoloni. Kwa hivyo, inapaswa kusemwa kwamba, makala hiyo, badala ya kutoa uchambuzi wa kweli na wa kimantiki, inatumika kuimarisha miradi ya kivita, ambayo gharama zake za kibinadamu na kiuchumi hulipwa na watu wa Asia Magharibi, na baadaye jamii ya kimataifa, haswa katika uwanja wa nishati.
Kama hakuna Iran, dunia itafanya nini?
Bila kujali yote yaliyosemwa, tunauliza tena kwamba, kama si Iran, nani atakayesimama mbele ya kiwango hicho kikubwa cha sera haribifu, mauaji, na ushawishi wa Israel kikanda na kimataifa?
Iran ni kikwazo dhidi ya tamaa na sera za kupenda kujitanua zisizo na mwisho za Israel, sio tu kwa ajili yake, bali kwa eneo zima la Asia Magharibi na dunia nzima kwa ujumla.
Dunia inapaswa kukubali kwamba Israel si dola halali, bali ni tishio kwa amani, usalama na ustawi wa kimataifa.