Abdollahian: Iran itaendelea kusimama pamoja na Syria hadi kutokomeza kabisa ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i101700-abdollahian_iran_itaendelea_kusimama_pamoja_na_syria_hadi_kutokomeza_kabisa_ugaidi
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza haja ya kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi ya Syria na kusisitiza kwamba, Iran itaendelea kusimama pamoja na Syria katika kukamilisha kampeni yake dhidi ya ugaidi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 31, 2023 08:44 UTC
  • Abdollahian: Iran itaendelea kusimama pamoja na Syria hadi kutokomeza kabisa ugaidi

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza haja ya kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi ya Syria na kusisitiza kwamba, Iran itaendelea kusimama pamoja na Syria katika kukamilisha kampeni yake dhidi ya ugaidi.

Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo katikka mazungumzo yake mjini Damascus na Rais Bashar al-Assad wa Syria ambapo aliwasili huko jana Jumatano akiongoza ujumbe wa Iran.

Hussein Amir-Abdollahian, ameongeza kuwa, kwa kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilisimama sambamba na Syria wakati wa kipindi kigumu cha  wa kampeni dhidi ya ugaidi, itaendeleza mtazamo huo huo katika kipindi hiki kipya cha kuelekea kuhitimishwa vita dhidi ya ugaidi na kujengwa Syria.

Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Iran amedokeza kuwa, maadui wa Syria bado wanatekeleza malengo yao ya kisiasa katika kukabiliana na nchi hiyo kupitia vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya serikali na wananchi wa Syria.

Rais Bashar al-Assad wa Syria

 

Mwanzoni mwa mazungumzo hayo, Rais Bashar Assad wa Syria aliipongeza serikali ya Iran na wananchi kwa kukubaliwa hivi karibuni uanachama katika kundi la BRICS na kuongeza, "Hii inaonyesha kuwa dunia inabadilika na kile ambacho wewe na mimi tulisimamia kilikuwa sahihi."

Bashar Assad ameuchukulia mkakati wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi kuwa sambamba na kulinda maslahi yake, unalenga kuibua na kuzusha migogoro na mivutano baina ya mataifa ya eneo hili, ikiwa ni pamoja na kuzusha mifarakano kati ya Shia na Sunni au Iran na Waarabu na akakaribisha mpango wa Iran wa kuimarisha uhusiano na nchi za Kiarabu za eneo na kuitaja kama hatua kubwa ya kimkakati.