Sep 25, 2023 06:10 UTC
  • Iran: Tunatangaza rasmi kuwa tuna makombora ya kuipiga Israel kutokea hapa hapa nchini

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi wa Iran amesema kuwa, leo hii Jamhuri ya Kiislamu ina makombora ambayo jina lake ni makombora ya kupiga Israel kwa sababu shabaha kubwa zaidi ya kubuniwa na kutengenezwa makombora hayo ni kuupiga utawala wa Kizayuni.

Shirika la habari la Tasnim limemnukuu Brigedia Jenerali Reza Talaei-Nik akisema hayo mjini Hamedan na kubainisha kwa uwazi nguvu kubwa za kiulinzi ilizo nazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa. 

Amesema, leo hii kila mtu anakiri kwamba, hakuna mlingano wowote wa ukanda wa Asia Magharibi unaoweza kufanyika bila ya kushirikishwa kikamilifu Iran.

Tunatangaza tena kwamba hatutoruhusu mabadiliko yoyote ya mipaka kwenye eneo hili. Huko nyuma adui hakuwa na uthubutu wa kufanya hivyo na katika siku za usoni pia hatothubutu.

Kombora la Hajj Qassem limeundwa maalumu kwa ajili ya kuipiga Israel

 

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi wa Iran amesema, hivi karibuni Jamhuri ya Kiislamu ilipata mafanikio mengine mapya katika upande wa kubuni na kutengeneza silaha akisisitiza kuwa, vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu (vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran) vimelipa taifa la Iran nguvu za kujiamini, kujitegemea na uwezo mkubwa wa kimaanawi wa kuwashinda maadui.

Brigedia Jenerali Talaei-Nik ameongeza kuwa, taifa la Iran litaendeleza njia ya mashahidi wa vita vya kujihami kutakatifu akisema kuwa, mashahidi wa Iran wametoka kwenye chuo cha Nabii Ismail AS ambaye amezaliwa na wazazi watukufu, Nabii Ibrahim na Bibi Hajar (AS) na kupata fakhari kubwa kupitia madhabahu ya Karbala ya Imam Husain AS.

Amesema, moja ya makombora ya kisasa kabisa ni lile linaloitwa Haj Qassem (la kuenzi jina la Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ambaye aliuliwa kidhulma na wanajeshi wa Marekani akiwa mgeni rasmi wa serikali ya Iraq) akisisitiza kwamba kombora hilo limeundwa kwa lengo la kuipiga Israel.