Pigo kubwa la Wizara ya Intelijensia kwa magaidi; kuzimwa makumi ya milipuko mjini Tehran
Wizara ya Intelijensia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kupitia taarifa kwamba imefanikiwa kuzima milipuko 30 ya wakati mmoja mjini Tehran na kuwatia mbaroni magaidi 28 waliokuwa wanapanga kuilipua na kusababisha maafa na hasara kubwa nchini.
Katika tangazo lake la jana Jumapili, wizara hiyo imesema: "Licha ya kwamba maajenti waliotiwa mbaroni ni wanachama wa Daesh, lakini muundo wa operesheni hiyo na mienendo ya magaidi hao ni ya kiufundi na kitaalamu zaidi kuliko miundo ya kawaida ya harakati za kitakfiri, na ina mafungamano makubwa zaidi na mbinu pamoja na mifumo inayotumiwa na utawala ghasibu wa Kizayuni. Kutumiwa mbinu za mkato zenye utaalamu mkubwa, mbinu za hadaa, ujanja, kushughulisha na kuwapotosha maafisa wa usalama, kulenga mawasiliano katika mitandao ya kijamii ya kigeni, hasa WhatsApp, kutumia vibaraka wa matabaka kadhaa katika mawasiliano, kutumia waghushi wenye utaalamu wa juu katika kupata nyaraka zinazohitajika na mambo mengine mengi katika uwanja huo, yote hayo yanathibitisha wazi uwepo wa vyanzo vingine muhimu nyuma ya pazia la vitendo vya magaidi wa Daesh waliokamatwa na maafisa usalama wa Iran."
Hapana shaka kuwa, mafanikio ya vikosi vya upelelezi na usalama vya Iran katika kugundua na kuzima mipango hiyo ya kigaidi yana nukta muhimu za kuzingatia. Mojawapo ni kwamba mafanikio hayo yanaashiria ubora wa juhudi za upelelezi na usalama za maafisa wa Iran, ukilinganishwa na wa maadui. Ubora huo wa kiwango cha juu cha upelelezi na usalama wa Iran, kama ulivyo uwezo wake wa kijeshi na kiulinzi, ni moja ya vipengele muhimu vya nguvu za nchi. Pigo dhidi ya mtandao mkubwa wa kigaidi na Kizayuni katika mikoa 4 ya Iran mwaka jana, pigo dhidi ya mtandao wa kupanga ghasia, kuzima na kuzuia hujuma ya shirika la ujasusi la Kizayuni (Mossad) katika sekta ya ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na vilevile kutiwa mbaroni magaidi 200 pamoja na kugunduliwa na kuteguliwa mabomu takriban 400 kote nchini mwaka huu ni moja ya mifano ya wazi ya mafanikio ya hivi karibuni ya mashirika ya upelelezi na usalama ya Iran.
Nukta nyingine muhimu ni kwamba, maadui sugu wa Iran kama vile Marekani na utawala wa Kizayuni ambao wametambua kwamba hawana uwezo wa kukabiliana kijeshi moja kwa moja na Iran, sasa wameamua kutumia zaidi vitendo vya ugaidi na kuibua ghasia nchini Iran kupitia mitandao ya kijamii. Kwa msingi huo wameanzisha vita mseto dhidi ya Iran kwa shabaha ya kuifanya Iran isiwe na amani na usalama. Kwa mtazamo huo, walikuwa wamepanga kulipua mabomu kadhaa ya wakati mmoja mjini Tehran kwa ajili ya kuvuruga usalama na kuonyesha sura bandia ya kutokuwepo utulivu nchini, kuibua hali ya kukata tamaa na hofu katika jamii na kuzusha machafuko na ghasia nchini, hasa kwa mnasaba wa kumbukumbu ya machafuko ya mwaka uliopita.
Wakati huo huo, ifahamike pia kwamba, ingawa maadui wametumia uwezo wao wote tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuyavunja au kwa uchache kuwakatisha tamaa wananchi kwa kuvuruga usalama wa taifa, lakini kutokana na mwamko na kuwa macho taifa pamoja na juhudi za maafisa wa upelelezi, usalama na jeshi la Iran katika nyuga hatari na nyeti za kulinda usalama na utulivu wa Iran ya Kiislamu, wamefanikiwa kuvunja njama kubwa na tata za mashirika ya kijasusi na kiusalama ya maadui na hivyo kuwafanya wasifikie malengo waliyokusudia.