Kan'ani: Azimio la mwisho la kikao cha wakuu wa nchi za Kiislamu nchini Saudi Arabia lina nguvu na thabiti
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema, mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamejumuishwa katika azimio la mwisho la kikao cha wakuu wa nchi za Kiislamu nchini Saudi Arabia, na ibara na maneno ya azimio hilo ni yenye nguvu na imara.
Nasser Kanani Chafi, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema hayo leo akijibu swali kuhusu azimio lililoidhinishwa na kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu mjini Riyadh na kuongeza kuwa: Mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wote wa mazungumzo yalijumuishwa kama hati katika azimio la mwisho, na ibara na maneno ya azimio hili ni thabiti na imara.
Msemaji huyo wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amebainisha vipengee vya azimio la kikao cha Riyadh na kueleza kuwa, kuzitaka serikali zote kusimamisha usafirishaji wa silaha kwa utawala wa Kizayuni, uamuzi wa haraka wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusimamisha vita, kuzuia uharibifu wa hospitali, kuondoa vizuizi vya kuingia kwa dawa, chakula na mafuta Gaza na kuondolewa mzingiro dhidi ya cha eneo hilo sambamba na kuruhusu kuingia misafara ya kibinadamu ya Kiarabu, Kiislamu na kimataifa, ni miongoni mwa mambo yaliyojumuishwa katika taarifa ya mwisho ya mkutano wa Riyadh.
Kikao cha dharura cha wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu kwa ajili ya kuitetea Palestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni kilifanyika Jumamosi mjini Riyadh, ambapo, Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasilisha mapendekezo kumi ya dharura kwa suala la Palestina, yakiwemo kusimamishwa mauaji ya watu wa Gaza, kuondolewa kikamilifu mzingiro na kufunguliwa vivuko, kuondoka mara moja jeshi la Kizayuni Gaza, kukatwa uhusiano wowote wa kisiasa na kibiashara na utawala wa Kizayuni na kutajwa jeshi la Kizayuni kuwa la kigaidi na serikali za Kiislamu.