Iran: Wanyonyaji damu wa Kizayuni wameanzisha upya mauaji Gaza kwa uungaji mkono wa US
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: baada ya kuwaua zaidi ya Wapalestina 15,000, wanyonyaji damu wa Kizayuni wameanzisha duru mpya ya mauaji huko Gaza kwa uungaji mkono kamili wanaoendelea kupewa na serikali ya Marekani.
Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, walikubaliana kusimamisha vita kwa siku nne kwa upatanishi wa Qatar, ambao ulianza Ijumaa iliyopita baada ya takribani siku 50 za vita, usitishaji vita ambao ulirefushwa mara mbili kwa siku mbili na hatimaye siku moja.
Lengo kuu la makubaliano hayo lilikuwa ni kubadilishana wafungwa na kupelekwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Leo Ijumaa, utawala wa Kizayuni umeanzisha duru mpya ya mashambulizi na mauaji ya Wapalestina dhidi ya Gaza.
Kufuatia hatua hiyo, Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria kitendo hicho cha utawala wa Kizayuni cha kuanzisha upya mashambulio ya kijeshi dhidi ya Gaza, mashambulio ambayo yalianza dakika chache kabla ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Anthony Blinken kuondoka Israel na kueleza kwamba: "kwa mara nyingine tena ni raia, watoto na wanawake ndio wahanga wakuu wa mashambulizi ya kijinai ya jeshi la Kizayuni".
Kanani ameongeza kuwa: mataifa na karibu nchi zote duniani zinapiga kelele zikitaka kuendelezwa usitishaji vita na kukomeshwa kikamilifu mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, lakini kwa dhana yao ya kipuuzi, Wazayuni wahalifu na wauaji wa watoto wanatafuta ushindi kwa kuua raia, watoto na wanawake ili kufidia kipigo ulichopata na kushindwa kusikoweza kufidika.
Msemaji wa vyombo vya kidiplomasia vya Iran amebainisha kwa kusema: ni wazi kuwa dhima ya kisiasa na kisheria ya kuendelezwa uvamizi na mauaji ya wananchi wa Palestina, mbali na kuwaelekea wahalifu wa utawala wa Kizayuni, inabebwa pia na serikali ya Marekani na serikali nyingine chache zinazouunga mkono utawala huo wa ubaguzi wa rangi wa Apathaidi.../