Dec 02, 2023 06:09 UTC
  • Iran yakanusha taarifa ya upotoshaji ya E3 kuhusu mpango wake wa makombora

Iran imekanusha ripoti ya upotoshaji na ya kisiasa ya Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani kuhusu uzinduaji wa kombora la Fattah-2.

Katika taarifa yake siku ya Ijumaa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani amesema madai ya nchi hizo tatu za Ulaya, zinazojulikana kama E3, kuhusu kombora hilo la Iran hayana msingi wa kisheria.

Amesema vikwazo vyote vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mpango wa makombora wa Iran vilisimamishwa tokea tarehe 18 Oktoba chini ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji wa 2015 (JCPOA). Kan’ani amesema, madai ya E3 dhidi ya mpango wa makombora wa Iran hayakubaliki na ni kinyume cha sheria.

Katika taarifa yao siku ya Alhamisi, E3 zimelaani kuzinduliwa kwa aina mpya ya kombora la balestiki la Iran mnamo Novemba 19 na kusema Iran inaendelea kuboresha mpango wake wa makombora licha ya wito wa mara kwa mara wa kimataifa wa kusitisha shughuli hiyo.

Baraza la Usalama

Pande hizo tatu za Ulaya katika mapatano ya JCPOA pia zimeishutumu Iran kwa kuvuruga amani na usalama wa eneo na dunia na kusema zitachukua hatua za kidiplomasia kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia.

Kan'ani amesema ustawi na uwezo wa makombora ya kujilinda wa Iran ni jambo linalofanyika kwa mujibu wa mahitaji ya kiulinzi ya nchi.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema, madai yasiyo na msingi, hayataathiri kwa vyovyote vile shughuli halali za ulinzi za Iran. Kana’ani ameishauri E3 kuepuka kutoa madai kama hayo ambayo yatadhuru uhusiano na ushirikiano kati ya Tehran na Ulaya.

Wataalamu na wahandisi wa kijeshi wa Iran katika miaka ya hivi karibuni wamefikia mafanikio muhimu katika utengenezaji wa aina mbalimbali za zana za kisasa, na kupelekea vikosi vya kijeshi kujitosheleza katika uwanja huo. Viongozi wa Iran wamekuwa wakisisitiza mara kwa mara kwamba Tehran haitasita kuimarisha uwezo wake wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa makombora, ambayo ni kwa ajili ya ulinzi wa taifa.