Kanani: Baadhi ya wanachama wa G7 ndio chanzo kikuu cha kukosekana utulivu Asia Magharibi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, baadhi ya wanachama wa kundi G7 ndio chanzo kikuu cha ukosefu wa amani na usalama katika Magharibi mwa Asia na duniani.
Nasser Kan'ani amelaani madai yasiyo na msingi yaliyotolewa katika taarifa ya "G7" dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa silaha za nyuklia hazina nafasi katika sera za ulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema: Shughuli za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ziko wazi kabisa, ni za amani na ziko ndani ya fremu ya haki na wajibu wa Iran kwa msingi wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.
Kan'ani ameyasema hayo baada ya kundi la G7 linalojumuisha nchi saba ambazo ni Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, na Uingereza kutoa tuhuma dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika taarifa yao kuhusu hali ya Gaza kwenye mkutano wa kilele uliofanyika chini ya uenyekiti wa Japan.
G7 pia imeitaka Iran kuacha kuziunga mkono harakati za Hamas, Hizbullah ya Lebanon na Ansarullah ya Yemen.
Akijibu madai na taarifa ya kundi hilo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria mchango na kuwajibika kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kusimamia na kuimarisha amani, utulivu na usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia na kusema: Baadhi ya wanachama wa kundi hili wana historia ya giza ya ukoloni, kubuni na kutekeleza sera haribifu na za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, kufanya mashambulizi ya kijeshi katika Asia ya Magharibi na maeneo mengine ya dunia, na zimesababisha ukosefu wa utulivu na usalama, si tu katika kanda hii, lakini pia duniani kote.
Nasser Kan'ani amesisitiza kuwa: Makundi ya muqawama katika eneo la Magharibi mwa Asia hayachukui amri kutoka kwa mtu yeyote kwa ajili ya kukabiliana na kujibu jinai za kivita na mauaji ya kimbari ya utawala unaoua watoto wa Israel.
Kan'ani aidha amelaani misaada na uungaji mkono kamili wa kijeshi wa Marekani na Uingereza kwa utawala wa Kizayuni wa Israel katika vita dhidi ya Palestina na kusisitiza ulazima wa kuwajibishwa nchi hizo kutokana na ushiriki wao katika jinai za kivita na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ghaza na Ukingo wa Magharibi.