Dec 08, 2023 13:27 UTC
  • Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Wanavyuo wamekuwa mstari wa mbele kupambana na ubeberu wa Marekani

Imamu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amesema wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran daima wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na ubeberu wa Marekani.

Ayatullah Sayyid Ahmad Hatami ameyasema hayo kwa mnasaba wa tarehe 16 Azar iliyosadifiana na Alkhamisi ya jana ambayo huadhimishwa kila mwaka nchini Iran kama "Siku ya Mwanachuo".   

Siku hiyo miaka 70 iliyopita, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran walifanya maandamano wakipinga safari ya Richard Nixon, Makamu wa Rais wa Marekani hapa nchini, na uingiliaji wa serikali ya Washington katika masuala ya ndani ya Iran. Maandamano hayo yalikandamizwa na jeshi la utawala kibaraka wa Shah ambapo wanafunzi watatu waliuawa shahidi na mamia ya wengine wakajeruhiiwa.

Akizungumzia tukio hilo, khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema, wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran daima wamekuwa katika safu ya mbele ya kupambana na ubeberu na kwamba nara ya "mauti kwa Marekani" ilitolewa kwa mara ya kwanza katika vyuo vikuu. 

Ayatullah Ahmad Hatami

Imamu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran ameashiria yanayojiri katika Ukanda wa Gaza na kueleza kuwa, stratijia ya Iran tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba Israel inapaswa kuondoka katika eneo la Magharibi mwa Asia, Palestina yni mali ya Wapalestina na kwamba uchaguzi unapaswa kufanyika ili kuamua hatma ya Palestina. Ayatullah Hatami amesema: Miaka 75 imepita tangu Israel ianze kufanya jinai dhidi ya watu wa Palestina na hii leo walimwengu wametambua usahihi wa stratijia hiyo ya Iran. Amesisitiza kuwa: Leo hii, hata katika nchi ya Uingereza, ambayo ilikuwa na nafasi katika kuanzishwa utawala bandia wa Israel, maelfu ya watu wanatoa nara ya "mauti kwa Israeli".

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema: "Wakati mmoja, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alikuwa akizungumzia suala la kubuniwa "Mashariki ya Kati Mpya", lakini leo hii, Mashariki ya Kati Mpya imeundwa kwa msingi wa muqawama ambao umevurunga mlingano wa nguvu katika eneo hilo."