Feb 26, 2024 03:04 UTC
  • Umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa shakhsia mashuhuri ambao daima wanasisitiza juu ya ushiriki mkubwa wa wananchi katika chaguzi tofauti zinazofanyika nchini.

Kuhusu ni kwa nini Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anatilia mkazo ulazima wa ushiriki huo mkubwa wa wananchi katika uchaguzi, tunapasa kufahamu kuwa, suala hili zaidi linahusiana na aina ya mtazamo na fikra zake kuhusu ushiriki katika uchaguzi.

Anachukulia ushiriki katika uchaguzi kuwa haki na wakati huo huo wajibu wa watu. Kuhusiana na hili, Ayatullah Khamenei anasema: 'Uwepo wa watu katika uchaguzi ni muhimu kwa maana halisi ya neno hili; yaani ni wajibu kwa watu na wakati huo huo ni haki yao. Mahudhurio ya watu kwenye uchaguzi si wajibu tu, bali ni haki. Ni haki yako, ni haki ya wananchi kumchagua mtu wanayemtaka kuwatungia sheria, kutekeleza sheria, kutoa maoni kuhusu Kiongozi Mkuu wa Mapunduzi au kumchagua Kiongozi huyo [kupitia] Baraza la Wataalamu. [Hii] ni haki ya watu; Wasimame na kutumia haki yao.'

Bila shaka, maoni kama hayo kuhusu ushiriki katika uchaguzi yanapotolewa, yanabainisha wazi umuhimu unaotolewa na shakhsia huyo kuhusu suala zima la uchaguzi. Ayatullah Khamenei ana mtazamo wa kisiasa kuhusu uchaguzi na anaamini kuwa uchaguzi una matokeo mengi ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi.

Kiongozi Muadhamu akizungumza karibuni mjini Tehran

Mtazamo wa kisiasa wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kuhusu uchaguzi unabainishwa wazi na matamshi na ibara ambazo amekuwa akizitoa nyakati tofauti kuhusiana na suala hilo. Kwa mfano amesema: 'Uchaguzi ni kutia damu mpya katika mfumo wa uendeshaji mambo ya nchi, uchaguzi ni dhihirisho la mamlaka ya kitaifa na uchaguzi ni Lailatul Qadr.' Ibara hizi zinaonyesha kuwa uchaguzi unaweza kuwa na athari chanya na hasi kwa hatima ya nchi. Kuchaguliwa wawakilishi wanaofaa hupelekea kuundwa bunge imara na lenye nguvu ambalo hatimaye hufanikiwa katika utekelezaji wa majukumu yake yakiwemo ya kutatua matatizo ya wananchi na kushughulikia changamoto zinazoikabili nchi. Kuchaguliwa wawakilishi dhaifu pia huwa na matokeo kinyume na hayo ambapo kimsingi hudhoofisha taasisi ya uchaguzi.

Aidha, uchaguzi huwa na matokeo muhimu ya kiusalama. Ushiriki mkubwa humaanisha uungaji mkono mkubwa wa wananchi kwa mfumo wa kisiasa, uungaji mkono ambao pia huwa ni mtaji wa kijamii na kisiasa wa nchi. Kadiri ushiriki wa watu unavyozidi kuwa mkubwa, ndivyo vitisho vya nje vikiwemo vya kijeshi na visivyokuwa vya kijeshi hupungua. Ushiriki unavyopungua pia ndivyo vitishio vinavyoongezeka. Kwa msingi huo, Ayatullah Khamenei anaufasiri uchaguzi kuwa ngome na kuamini kuwa uchaguzi ni ngao kwa sababu unazuia uchokozi na uingiliaji wa adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi anasema kuhusiana na hilo: “Kushiriki katika uchaguzi ni mojawapo ya njia muhimu zaidi zinazoweza kulinda taifa, mithili ya ngao ya chuma inayotumiwa na askari kujilinda mbele ya mashambulizi na hujuma ya maadui wenye nia mbaya. Uchaguzi ni muhimu sana."

Ibara na matamshi haya yanayotumiwa na Ayatullah Khamenei kuhusiana na uchaguzi yanathibitisha wazi umuhimu wa uchaguzi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Yanabainisha pia kwamba, tofauti na zilivyo nchi nyingi duniani, uchaguzi nchini Iran si wa kimapambo na kujionyesha tu, bali ni wa maamuzi yanayoleta mabadiliko ya msingi.

Tags