Feb 29, 2024 07:14 UTC
  • Ukosoaji wa Iran kwa Baraza la Usalama la UN kwa kutochukua hatua kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Ghazza

Tangu ilipoanza duru mpya ya mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghazza, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitumia kila fursa inayopata kulaani jinai za utawala huo ghasibu na kutaka mashambulizi ya kinyama yanayofanywa dhidi ya Wapalestina yakomeshwe.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian siku ya Jumatatu alihutubia kikao cha kujadili kadhia ya Palestina kilichofanyika pembeni ya kikao cha 55 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, ambapo sambamba na kukumbusha kuwa, karibu miezi mitano imepita tangu utawala wa Israel ulipoanzisha mashambulizi dhidi ya Ghazza na mauaji ya kimbari katika eneo hilo alisema, katika kipindi hicho, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi zinazojinasibu kuwa watetezi wa haki za binadamu hazijachukua hatua za maana kukomesha jinai za Israel.
Amir-Abdollahian aliongeza kuwa, tunachoshuhudia hii leo kutokana na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutochukua hatua kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Wapalestina huko Ghazza, ni "Janga la Kidiplomasia la Karne"; na kuendelea jinai za kivita za Israel pamoja na matokeo ya hatua ya Marekani na Magharibi ya kupanua wigo wa vita hivyo, ni tishio halisi kwa amani na usalama wa kimataifa.
Ukosoaji wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa Baraza la Usalama la UN kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Wapalestina 

Hadi sasa Wapalestina wapatao 30,000 wa Ukanda wa Ghazza wameuawa shahidi na wengine karibu 70,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na Wazayuni katika eneo hilo, ambapo asilimia 70 kati ya waliouawa ni wanawake na watoto. Kwa mujibu wa ripoti za kimataifa, mauaji ya Wapalestina huko Ghazza ni aina ya kutisha zaidi ya mauaji ya kimbari na ya watoto kuwahi kushuhudiwa katika historia ya wanadamu. Juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na baadhi ya nchi pamoja na taasisi za kimataifa za kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghazza zinafanywa huku Wazayuni hao, wakiungwa mkono na Marekani, wakiwa wanaendeleza jinai zao; na hivi sasa wanajipanga kuzusha janga na maafa mengine ya kutisha katika mji wa mpakani wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghazza.

Baada ya Wapalestina wapatao milioni moja na nusu wanaoishi katika maeneo tofauti ya Ghazza kuyahama makazi yao kutokana na mashambulio ya kinyama ya jeshi la Kizayuni na kukimbilia kwenye mji wa mpakani wa Rafah kusini mwa ukanda huo, hivi sasa utawala wa Kizayuni umetangaza kuwa unajipanga kufanya uvamizi na mashambulio mengine mapya kwa lengo la kuwaangamiza wapiganaji wa harakati ya Hamas katika eneo hilo. Mashirika ya kutetea haki za binadamu, bali hata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa iwapo Rafah itashambuliwa, dunia itashuhudia mauaji makubwa zaidi ya kimbari ya Wapalestina.

Jinai za Wazayuni Ghazza

Katika hali hiyo, badala ya Marekani na Uingereza kufanya jitihada za kusimamisha vita na mauaji ya Wapalestina wasio na hatia, nchi hizo mbili ambazo ndio waungaji mkono wakuu wa jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni, zimeendelea kuupatia silaha utawala huo sambamba na kuyapigia kura za turufu maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kusitisha vita huko Ghazza na hivyo kudhihirisha waziwazi uungaji mkono wao kwa mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa katika eneo hilo.

Uungaji mkono wa Magharibi kwa jinai za Wazayuni unaonyesha vipimo vya kiundumakuwili unavyotumia kuhusiana na suala la Palestina; na kwa hakika vita vya Ghazza vinadhihirisha unafiki wa Magharibi katika uga wa haki za binadamu kwenye kipindi hiki nyeti na muhimu.

Licha ya misukosuko na masaibu yote yanayowafika Wapalestina, kipindi hiki cha hali ngumu mno wanachokipitia wananchi hao madhulumu kitamalizika; lakini historia itasajili na kuweka kwenye kumbukumbu zake namna nchi mojamoja na kila taasisi ya kimataifa ilivyochukua msimamo kuhusiana na mauaji dhahiri ya kimbari yanayofanywa huko Ghazza.

Kwa hakika mauaji ya Wapalestina, hususan wa  Ukanda wa Ghazza, hayawezi kuendelea kadiri watakavyopenda Wazayuni na waungaji mkono wao, kwa sababu katika historia hakuna taifa lolote lililoridhia kupoteza ardhi yake, na vivyo hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa Palestina pia.

Jinai za Wazayuni Ghazza

Ni kwa sababu hiyo, ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua msimamo wa kulitetea taifa la Palestina dhidi ya uvamizi na kukaliwa ardhi zake kwa mabavu, kwa kufuata misingi ya sheria za kimataifa na haki ya kila taifa kujiamulia mustakabali wake; na inaitakidi kwamba, juhudi zote za kieneo na kimataifa zitakazofanywa kutatua kadhia ya Palestina ni lazima zizingatie na kutilia maanani ukweli kwamba ardhi ya Palestina ni milki ya watu wa Palestina; na kwa hivyo uamuzi wowote kuhusu mustakabali wa ardhi hiyo lazima ufanywe na Wapalestina wenyewe.../

Tags