May 28, 2024 08:29 UTC
  • Kuanza mchakato nchini Iran wa kufanyika uchaguzi wa Rais wa kabla ya wakati

Iran imeanzisha mchakato wa uchaguzi wa mapema wa rais ambao umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Juni.

Mchakato huo umeanza wiki moja baada ya Rais Ebrahim Raisi kufa shahidi katika ajali mbaya ya helikopta kaskazini magharibi mwa nchi mnamo Mei 19.

Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmad Vahidi alitoa amri siku ya Jumapili akiwaamuru magavana wa majimbo na miji kote Iran kuunda kamati kuu za uchaguzi ndani ya siku tatu zijazo kwa minajili ya kufanyika duru ya 14 ya uchaguzi wa Rais hapa nchini.

Uchaguzi wa mapema wa urais unafanyika ili kutekeleza kifungu cha 130 cha Katiba ya Iran na vilevile sheria ya uchaguzi wa Rais.

Baraza linalojumuisha wakuu wa mihimili mitatu ya serikali ya Iran lilifanya mkutano siku moja baada ya kuaga dunia shahidi Ebrahim Raisi na kukubaliana Juni 28 kuwa tarehe ya uchaguzi wa mapema wa rais nchini.

Helikopta iliyokuwa imembeba Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumapili jioni Mei 19, 2024 ilipata ajali ilipokuwa ikirejea kutoka kwenye hafla ya ufunguzi wa bwawa la Qiz Qalasi kwenye mpaka wa pamoja wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.

Wakati helikopta hiyo ilipokuwa inaelekea mji wa Tabriz, ilianguka katika eneo la Varzghan mkoani Azarbaijan Mashariki, kaskazini-magharibi mwa Iran. Ndani yake walikuwemo pia Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Imam wa Ijumaa wa Tabriz, Gavana wa Azarbaijan Mashariki na watu wengine; na wote pamoja wakapata hadhi tukufu ya kufa shahidi.

Makao Makuu ya Uchaguzi ya Iran yalitoa notisi ya kwanza Jumapili yakitangaza kwamba wagombea wanaweza kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi kati ya Mei 30 na Juni 3.

 

Baraza la Walinzi wa Katiba la Iran, chombo muhimu cha usimamizi wa kikatiba na kidini kinachohusika na usahihi wa uchaguzi, kitatangaza orodha ya wagombea walioidhinishwa wiki mbili kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza.

Kampeni zitaanza Juni 12 na kuendelea hadi Juni 27.

Kuwa raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuwa na faili la usimamizi na uongozi mzuri, kuamini misingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na madhehebu rasmi ya nchi ni miongoni mwa sifa muhimu wanazopaswa kuwa nazo wagombea wanaowania kiti cha urais nchini Iran.

Katika kalenda ya matukio ya uchaguzi wa Iran; duru kumi na tatu za uchaguzi wa rais zimesajiliwa hadi sasa, na duru ya 14 ya chaguzi hizi, ambayo ilipaswa kufanyika mwaka ujao, itafanyika mwezi ujao, ikiwa ni mwaka mmoja mapema, kutokana kufa shahidi Rais wa serikali ya awamu ya 13.

Utayari wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na taasisi nyingine za Jamhuri ya Kiislamu wa kufanya uchaguzi wa rais ndani ya siku 50 unaonyesha uwezo wa nchi katika kukabiliana na changamoto katika mazingira maalumu na nyeti ya eneo, mfano kama huu unapatikana katika nchi chache duniani.

Kuteuliwa Ayatullah Ali Khamenei kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu saa chache tu baada ya kutangazwa kifo cha Imam Khomeini (RA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu, ni kielelezo tosha cha utayarifu wa nchi kusimamia ipasavyo hali ya mambo katika hali maalumu, ambayo miaka 35 iliyopita ilisifiwa na viongozi wengi na shakhsia wa kimataifa na kuleta mshangao pia baina yao.

Pamoja na hayo inapasa kukiri kwamba, uchaguzi wa rais ni muhimu zaidi kuliko uchaguzi wa wabunge na mabaraza ya Kiislamu nchini Iran. Hii ni kutokana na kuwa, chombo cha utendaji wa nchi yaani serikali ndicho chenye dhamana ya usimamizi na wajibu mkubwa hususan katika uga wa sera za kiuchumi na za kigeni.

 

Usimamizi na uongozi muhimu na wenye taarhira zaidi wa nchi ni urais. Ni kwa kuzingatia uhalisia huo, ndio maana ushiriki wa asilimia kubwa zaidi wa wananchi katika uchaguzi wa rais ni uainishaji wa hatima na maamuzi na kwa hakika unadhamini uhalali na kukubalika kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Tajiriba ya miaka 45 ya historia ya Mapinduzi ya Kiislamu iko wazi kwa kila mtu kwamba, kila mara wananchi waliposhiriki kwa shauku na hamasa kubwa katika medani muhimu za kisiasa hususan katika uchaguzi, mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ulifanikiwa kuvuka kwa mafanikio matatizo na changamoto na hivyo kudhamini maslahi ya kitaifa sambamba na kukidhi matakwa ya wananchi.

Kwa maneno mengine ni kuwa, uungaji mkono wa watu ndio sehemu muhimu zaidi ya kujenga mamlaka na kuongeza nguvu za kitaifa, na kwa upande mwingine, inauthibitishia ulimwengu kwamba utawala na uongozi nchini Iran unapatikana kwa njia ya uchaguzi na matakwa na ridaha ya wananchi ni mambo yaanayozingatiwa na kupewa nafasi na umuhimu katika uongozi.

Kuvuka salama vipindi vigumu katika kipindi cha miaka 45 iliyopita, ikiwa ni pamoja na miaka minane ya vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq wa dikteta Saddam dhidi ya Iran, vikwazo vya pande zote vya Marekani, kusambaratisha njama mbalimbali za maadui na kugongwa mwamba sera za Marekani za mashinikizo ya kiiwango cha juu kabisa, yote hayo chimbuko lake ni wananchi kuwa pamoja na bega kwa bega na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unaotawala hapa nchini.

Mintarafu hiyo, inatarajiwa kwamba mwezi ujao wananchi wa Iran watajitokeza kwa wingi ambapo sambamba na kuthamani huduma za serikali ya awamu ya 13 hususan Rais Ebrahim Raisi na baraza lake la mawaziri, watatangaza tena himaya na uungaji mkono wao kwa serikali mpya itakayotokana na kura za wananchi.

Tags