Kufafanuliwa na Rais mteule Masoud Pezeshkian fremu ya sera za kigeni za serikali mpya ya Iran
Katika risala yake ya pili, rais mteule wa Iran Masoud Pezeshkian, amefafanua sera ya serikali mpya katika uga wa nje.
Katika siku za hivi karibuni, Daktari Masoud Pezeshkian Rais Mteule wa Iran, ambaye alichaguliwa kuwa rais mpya wa Iran kwa kura za wananchi mwezi Julai tarehe 5, mwaka 2024, alitoa risala mbili kuhusu sera ya kigeni ya serikali mpya.

Katika dondoo ya kwanza iliyochapishwa na gazeti la Qatar "Al Arabi Al-Jadid" kwa anuani ya "Pamoja kwa ajili ya Eneo Imara na lenye Ustawi", alisisitiza juu ya kustawishwa ushirikiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na majirani zake.
Kwa hakika sera za kieneo za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika serikali mpya ni muendelezo wa stratijia ya serikali ya Rais shahidi Sayyid Ebrahim Raisi.
Kuhusiana na suala hili, Daktari Masoud Pezeshkian Rais Mteule wa Iran; katika makala yake hii aliyoyaandika, amesisitiza kuwa, kipaumbele cha sera za kigeni za Iran ni kupanua ushirikiano na majirani na uhusiano huo uwe kwa msingi wa kuheshimiana pande mbili na vilevile kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na ardhi yote ya mataifa. Katika Makala yake ya pili, iliyochapishwa na gazeti la Tehran Times, Pezeshikian amesisitiza udharura wa kuendelezwa ushirikiano wa Iran na mataifa ya Russia na China. Aidha katika sehemu nyingine ya Makala yake hii, rias mteule wa Iran sambamba na kutilia mkazo suala la kuimarisha ushirikiano na mataifa jirani amesema kuwa, Tehran itashirikiana na Ulaya pia. Amesema, kufanya mazungumzo yenye kujenga na Ulaya ni kipaumbele muhimu na kikuu cha serikali mpya.

Aidha katika sehemu nyingine ya makala yake hiyo ni kuhusu uhusiano wa Iran na Marekani.
Nukta nyingine muhimu katika suala hili ni kwamba Daktari Rais Masoud Pezeshkian Rais Mteule wa Iran, alisisitiza kwamba; Marekani inapaswa kutambua ukweli na kujua vyema na daima kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijakubali na haitasalimu amri kamwe mbele ya mashinikizo.
Mbali na kadhia zilizotajwa ambazo zinahusiana na uhusiano na majirani na nchi za nje ya kikanda, katika maelezo yake Masoud Pezeshkian Rais Mteule wa Iran, alisisitiza kwamba, msingi wa siasa za nje za serikali mpya ya Iran umejikita katika misingi mitatu ya heshima, hekima na maslahi.
Wakati huo huo, katika maelezo yake, Daktari Rais Masoud Pezeshkian Rais Mteule wa Iran, amezitambulisha sera za kigeni kama uwanja wa fursa na ni wazi kwamba anaona sera ya kigeni kama fursa ya maingiliano na mashirikiano.
Kwa msingi huo basi, katika uwanja wa sera za kigeni, kwa upande mmoja, anafuatilia suala la kuweko usawa na uwiano katika uhusiano na nchi zote, na kwa upande mwingine, anafuatilia maslahi ya kiuchumi katika sera ya kigeni, na kupitia njia hiyo anafanya juhudi kufuatilia masilahi ya kiuchumi ya Iran katika uga wa kieneo na nje ya eneo hili.
Kwa msingi huo tunaweza kusema kwamba, ujumbe wa rais mteule wa Iran katika uga wa sera za kigeni ni kuchukua mkondo wa sera za mlingano sambamba na kutoa kipaumbele maslahi ya kiuchumi ya Iran na wakati huo huo kukaribisha kwa mikono miwili suala la kupanua uhusiano na mataifa yote.