Aug 03, 2024 10:54 UTC
  • Iran: Kimbunga cha hasira za wapenda haki kitaukumba utawala wa Kizayuni wa Israel karibuni hivi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezungumzia jinsi utawala wa Kizayuni unavyoendelea na jinai zake na kusema kuwa, karibuni hivi utawala huo dhalimu utakumbwa na kimbunga cha hasira za mataifa na tawala zinazopenda haki na uadilifu duniani.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Nasser Kan'ani akisema hayo katika mtandao wa kijamii wa X na kuandika: "Utawala wa Kizayuni ni tishio halisi la usalama, utulivu na amani ya dunia nzima kutokana na kuendelea kwake na jinai za kivita na mauaji ya kizazi huko Palestina na kutokana na kiburi chake cha kuvunja waziwazi haki ya kujitawala nchi mbalimbali sambamba na vitendo vyake vya kigaidi kieneo na kimataifa. Mbegu ya hasira na chuki za walimwengu, wananchi wa Palestina n.k, dhidi ya utawala wa Kizayuni inazidi kumea na kunawiri."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, karibuni tu hivi utawala muovu, mbaguzi wa rangi na uliofurutu ada wa Israel utakumbwa na kimbunga kisichozuilika cha moto wa hasira za wapenda haki duniani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani 

 

Miongoni mwa jinai za karibuni kabisa za utawala wa Kizayuni wa Israel, ni kuwaua shahidi na kidhulma Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Fuad Shukr, mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa Hizbullah ya Lebanon, jambo ambalo limeufanya utawala wa Kizayuni ujiweke karibu zaidi na kuangamia kwake. 

Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS aliuawa shahidi hapa Tehran, usiku wa kuamkia Jumatano ya tarehe 31 Julai, baada ya nyumba aliyofikia kushambuliwa na vibaraka wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Haniyeh alikuja Tehran kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais wa awamu ya 14 ya serikali ya Iran.