Rais Pezeshkian: Kuimarisha uhusiano na Russia ni 'kipaumbele cha sera za nje' kwa Iran
Aug 06, 2024 03:23 UTC
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaja Russia kuwa ni "mshirika wa kimkakati" wa Jamhuri ya Kiislamu, akisisitiza kwamba kupanuliwa uhusiano na Moscow ni kipaumbele cha juu cha sera za nje za serikali yake.
Pezeshkian ameyasema hayo jana Jumatatu alipokutana na Katibu wa Baraza la Usalama la Russia Sergei Shoigu ambaye alikuwa mjini Tehran kwa ziara ya siku moja ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Iran.
Amebainisha kuwa, Russia imekuwa mshirika thabiti katika nyakati za changamoto kwa Iran na kusisitiza ulazima wa kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi hizo mbili.
"Tunaamini kwamba enzi ya maamuzi ya upande mmoja yanayochukuliwa na madola fulani ikiwemo Marekani, imekwisha," amesema Rais Pezeshkian na kubainisha kuwa: "Mfungamano wa misimamo na ushirikiano kati ya Iran na Russia katika kujenga ulimwengu wa pande kadhaa bila shaka utaimarisha usalama na amani duniani."
Ziara ya Shoigu hapa hapa nchini imefanyika huku kukiwa na mvutano mkubwa katika eneo hili la Asia Magharibi baada ya utawala wa kigaidi wa Israel kumuua Ismail Haniya, kiongozi wa kisiasa wa Hamas, mjini Tehran siku ya Jumatano iliyopita, na kulisukuma eneo kwenye ukingo wa vita.
Tehran imeapa kwamba kitendo cha uchokozi kilichofanywa ndani ya ardhi yake hakitapita bila jibu.
Rais Pezeshkian alisisitiza jana kwamba mauaji ya Shahidi Ismali Haniya ni ukiukaji wa wazi wa sheria na kanuni za kimataifa.
Alisema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki kwa vyovyote kupanua wigo wa vita na mgogoro katika eneo, lakini kwa hakika utawala huu utapata jibu kwa jinai na uthubutu wake".
Moscow pia imelaani vikali mauaji ya Haniya, ambaye alikuwa mhusika mkuu katika mazungumzo ya kusitisha mapigano Ghaza. Maafisa wakuu wa Russia wamesema, wale waliohusika na mauaji hayo wamelenga kuvuruga matumaini yote ya kurejesha amani katika eneo hili na kuivuta Marekani iingie kwenye makabiliano na Iran.
Kwa upande wake Shoigu amempongeza Pezeshkian kwa mara nyingine tena kwa kuchaguliwa kuwa rais wa Iran na akaitaja Jamhuri ya Kiislamu kuwa mshirika mkuu wa kistratijia wa Russia katika eneo.
Akielezea kuridhishwa na juhudi za pamoja za Russia na Iran za kuunda "ulimwengu wa kambi kadhaa" na kuhakikisha usalama wa kikanda, alisisitiza kwamba uhusiano kati ya washirika hao wawili unakua katika sekta zote.
Kabla ya kukutana na Rais Pezeshkian, Shoigu alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri.../