Naibu Waziri wa Kazi wa Oman: Iran ni mahala salama kwa wawekezaji wa Oman
(last modified 2024-09-09T06:52:40+00:00 )
Sep 09, 2024 06:52 UTC
  • Naibu Waziri wa Kazi wa Oman: Iran ni mahala salama kwa wawekezaji wa Oman

Naibu Waziri wa Kazi wa Oman amesisitiza kuwa Iran ni mahali salama kwa wawekezaji wa Oman kutokana na usalama na miundombinu yake mwafaka.

Ahmed bin Salem Al Hajari ameyasema hayo katika mahojiano maalum na IRNA kando ya ziara yake aliyofanya jana Jumapili ya kutembelea Eneo Huru la Uwekezaji la Arvand.
 
Amesema, kuna fursa nzuri nchini Iran katika nyanja mbalimbali zikiwemo za viwanda, afya na utalii ili kuvutia wawekezaji wa kigeni, na kutokana na kuweko maeneo huru na maalumu ya uwekezaji katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wawekezaji wa Oman wanaweza kuwekeza hapa nchini na kutumia fursa ya misamaha ya kodi.
 
Naibu Waziri huyo amesema pia kuwa Iran ni nchi rafiki na ndugu kwa Oman, na uhusiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili umepelekea kuwepo uwekezaji wa dola bilioni mbili hadi sasa.
 
Al-Hajari ameongeza kuwa, serikali ya Oman imetoa masharti maalumu na ya gharama nafuu kwa wawekezaji wa Iran hususan katika maeneo 14 huru na maalumu ya kiuchumi kwa kutoa mabadilishano ya kiuchumi na kupunguza kodi.

Kulingana na afisa huyo, Oman inatoa suhula nzuri kwa wafanyabiashara wa kigeni, hasa Wairani.

 
Amebainisha pia kuwa sekta ya Iran ya uwekezaji inakabiliwa na vikwazo na kwa hivyo Oman iko tayari kushirikiana na nchi hiyo rafiki.
 
"Serikali ya Oman iko tayari kushirikiana na wawekezaji wa Iran katika nyanja za sekta ya afya, usalama wa chakula, na madawa" ameeleza naibu waziri huyo wa Oman.
 
Aidha, Al-Hajari amependekeza sheria ya kazi na uwekezaji ya Iran iwape motisha wawekezaji wa Oman kwa ajili ya kuwekeza katika Eneo Huru la Arvand.
 
Licha ya mivutano iliyozuka katika eneo la Ghuba ya Uajemi sambamba na njama za Marekani za kushadidisha chuki na hofu kuhusiana na Iran, katika miaka ya karibuni uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman daima umekuwa ukiendelezwa juu ya msingi wa kuheshimiana na kuzingatia maslahi ya pande mbili.
 
Viongozi wa Oman wanaamini kuwa uhusiano wa karibu uliopo kati ya nchi yao na Iran unatokana na kuzingatia uhalisia na wanaichukulia Iran kama jirani mkubwa.
Nchi hizo mbili hazina mizozo ya kieneo wala ya mipaka baina yao, na uungaji mkono wa Iran kwa Oman umekuwa na sura chanya na ya kudumu katika kumbukumbu za historia ya nchi hiyo.../

 

 

Tags