Iran yapendekeza muungano wa kupambana na vikwazo ili kuhakikisha usalama wa biashara katika BRICS
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran (SNSC) Ali Akbar Ahmadian ametoa wito wa kuanzishwa muungano wa kukabiliana na vikwazo ili kukuza biashara na usalama wa kifedha kati ya kundi la BRICS la nchi zinazoinukia kiuchumi.
Ahmadian ametoa pendekezo hilo katika mkutano wa pamoja wa maafisa wa ngazi za juu wa usalama kutoka nchi za kundi la BRICS na Global South katika mji wa Saint Petersburg nchini Russia.
Mkuu huyo wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran amesema ni muhimu kwa BRICS na nchi za Kusini mwa Dunia kushikana mikono ili kuhakikisha usalama katika nyanja mbalimbali kwa misingi ya ulimwengu wa kambi kadha na utaratibu mpya wa dunia.
“Usalama wa kiuchumi na kushughulikia vikwazo vya usalama wa nishati, usalama wa chakula, usalama wa fedha, usalama wa kiuchumi, usalama wa usafirishaji wa baharini, usalama wa kiutamaduni, usalama wa kisaikolojia, usalama wa mtandao, usalama wa mazingira, usalama wa afya na usalama wa kimataifa, kwa ujumla, unahitaji ushirikiano wa pamoja wa BRICS na nchi za Kusini mwa dunia ili kuharakisha mabadiliko ya kimuundo na uundaji wa taasisi zenye ufanisi na za kisasa kulingana na utaratibu mpya wa dunia haraka iwezekanavyo," amesema Ahmadian .
Akiangazia umuhimu wa muungano wa kukabiliana na vikwazo, Ahmadian ameongeza: “Mtazamo huu wa BRICS na nchi za Kusini mwa Dunia utakuwa na jukumu kubwa katika kuunda usalama wa kiuchumi, kibiashara na kifedha na kuanzisha utaratibu wa kupambana utakatishaji fedha.”
Akigusia kuongezeka kwa hamu ya kimataifa ya kuwepo ulimwengu wa kambi kadhaa, afisa mkuu wa usalama wa Iran amesema, miundo na mashirika mengi yaliyopo yameshikiliwa mateka na Marekani kwa miaka mingi.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa la Iran amesema: "Miundo na taasisi za kimataifa zimechukuliwa mateka na Marekani na washirika wake," na sio tu kwamba zimethibitisha kutokuwa na ufanisi katika kuimarisha amani na utulivu wa kudumu duniani, lakini pia" zinatumia mkakati wa Washington kupanua ugaidi na vikwazo na kuunda hali ya wasiwasi katika ngazi ya kimataifa.”
Ahmadian amesisitiza kuwa mfumo wa kimataifa uko kwenye njia ya mpito kutoka ulimwengu wa kambi moja hadi ulimwengu wa haki zaidi na kuibuka kwa mfumo wa kambi nyingi na ushirikiano.