Sep 13, 2024 11:45 UTC
  • Khatibu wa Sala ya Ijumaa Tehran: Umoja ni kipaumbele cha ulimwengu wa Kiislamu

Khatibu wa muda wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema: "Umoja ni moja ya vipaumbele vya Ulimwengu wa Kiislamu na  ndiyo maana silaha muhimu ya adui katika kueneza ukoloni ni kuibua mifarakano."

Katika khutba zake za Swala ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran, Ayatullah Kazem Siddiqui amesema: "Natuma salamu za pongezi kwa mnasaba wa kukumbuka kuzaliwa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, mleta dini kamilifu ya Mwenyezi Mungu, Muhammad Ibn Abdullah (SAW)."

Ayatullah Siddiqui amesema kuna Waislamu wanaoamini kuwa Maulid au siku ya kukumbuka kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) ni tarehe 12 Rabi ul Awwal na wengine wanaamini siku hiyo ni  17 Rabi ul Awwal na kuongeza kuwa : "Tunakubali riwaya zote mbili".

Akiashiria Wiki ya Umoja wa Kiislamu ambayo huadhimishwa katika muda ulio baina ya siku hizo mbili, Ayatullah Sidddiqui amesema: "Umoja ni sawa kama uhai. Mfarakano na mgawanyiko katika jamii ni ishara ya kifo chake, lakini umoja ni ishara ya jamii kuwa hai."

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesema kulinda uwepo wa Umma wa Kiislamu katika katika upeo wake wa kijiografia, kuhifadhi heshima ya Umma wa Kiislamu na kuimarisha uwezo wa umma pamoja na juhudi za kuongeza utajiri wa kiuchumi wa nchi za Kiislamu na kadhia ya umoja ni miongoni mwa vipaumbele vya Ulimwengu wa Kiislamu.

Aidha amewataka Waislamu kuwa macho na kusema: "Leo adui yuko vitani na  Uislamu, na wala adui hajali iwapo Mwislamu anayelengwa ni Shia au Sunni."