Ubalozi wa Iran London kwa Wamagharibi: Zungumzeni na Iran kwa lugha ya heshima
Ubalozi wa Iran mjini London huko Uingereza umezungumzia tukio la kurushwa angani kwa mafanikio satelaiti ya utafiti ya "Chamran-1" na maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu katika tasnia ya anga za juu licha ya vikwazo visivyo vya haki vya nchi za Magharibi na kusema: Zungumzeni na Iran kwa lugha ya heshima, na si kwa lugha ya vikwazo.
Ubalozi wa Iran mjini London umeandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Iran imefanikiwa kutuma satalaiti yake ya masuala ya utafiti, Chamran-1, katika anga za mbali. Wakati umepita ambapo Iran ilikuwa ikitafuta kombora moja tu kutoka nchi moja hadi nyingine ili kujilinda, lakini leo, licha ya vikwazo, inatuma satelaiti yake ya kisasa zaidi katika angani za mbali."
Ujumbe huo umeongeza kwa kuziambia nchi za Magharibi: Kwa hivyo, zungumzeni na Iran kwa lugha ya heshima na sio kwa lugha ya vikwazo.
Awali, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran alisema kuwa, kurushwa satelaiti ya utafiti ya Iran iliyopewa jina la "Chamran-1" katika anga za mbali kwa mafanikio ni pigo kwa maadui wanaoliwekea taifa hili vikwazo visivyo na mantiki.
Nasser Kana'ni amesema katika ujumbe alioutuma kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X kwamba, kwa kurushwa kwa mafanikio satelaiti ya utafiti ya Chamran-1 kwa kutumia chombo cha kubeba satelaiti cha Qaem 100 na kuwekwa kwenye mzunguko wa kilomita 550 wa dunia ni baraka kwa Wairani wote, wanasayansi wa Iran, na wasomi haswa wale waliohusika katika mafanikio haya ya kujivunia.
Amewahutubu Wamagharibi kwa kuwaambia, "Waweka vikwazo wasio na mantiki kwa mara nyingine tena wamepewa jibu la vitendo vyao visivyo na mantiki."
Kan'ani amesema, Iran ni mdau mwenye mantiki, mwenye nguvu na mwenye kujenga na kuongeza kuwa, ni bora kwa Wamagharibi kutathmini upya mienendo ya matamshi yao.