Sep 17, 2024 13:00 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Sera za kindumakuwili za Magharibi zimedhihirika katika Michezo ya Olimpiki na Paralimpiki ya Paris

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamanei, ameeleza kuchuuzwa kwake na sera za kinafiki na kindumakuwili zinazotumiwa na nchi zinazosimamia mashirikisho ya kimataifa ya michezo na kusema kuwa, sera hizo mbovu zilidhihirika wazi wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto ya 2024 na Michezo ya Olimpiki ya Walemavu iliyomalizika hivi karibuni katika mji mkuu wa Ufaransa, Paris.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo Jumanne katika kikao chake na washindi wa medali, wanamichezo, makocha na wasimamizi wa wajumbe wa michezo wa Iran katika majukwaa ya michezo ya kimataifa.

Amesema sera za undumakuwili na upendeleo za nchi zinazosimama michezo ya kimataifa zimehisika na kuoneka wazi zaidi katika kipindi hiki cha mashindano ya Olimpiki na Paralimpiki na kuongeza kuwa: Wakati baadhi ya nchi zinazuiwa kushiriki mashindano hayo kutokana na vita, utawala wa Kizayuni wa Israel umeruhusiwa kushiriki kwenye mashindano hayo ya kimataifa licha ya kwamba katika kipindi cha karibu mwaka mmoja sasa umeua wanaadamu elfu 41 wakiwemo maelfu ya watoto.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Siasa hizi za kindumakuwili na upendeleo, kama ilivyosemwa mara nyingi, zinaonyesha kuwa kinyume na madai kwamba siasa haziingizwi kwenye michezo, hatua  nyingi zinazochukuliwa katika michezo zina malengo ya kisiasa.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja mashindano ya kimataifa kuwa ni jukwaa la kuonyesha nguvu za kiroho na kujiamini kwa mataifa mbalimbali, sambamba na nguvu za kimwili na umahiri wa kimichezo, na kuongeza kuwa: Wanamichezo wa Iran mbali na kuonyesha uwezo wao wa kitaaluma na kimichezo, wamewadhihirisha maadui uwezo wao wa kiroho na utambulisho wa kitaifa, kidini na Kiislamu kupitia vitendo vyenye maana maalumu kama vile kuwatunuku watoto wa Palestina na Gaza medali zao, kuvaa hijabu na vazi la staha, kuupa msafara wa wanamichezo wa Iran majina ya Maimamu watoharifu (a.s.) na kupiga picha za selfi wakiwa na bendera ya Palestina.

Wanariadha wa Iran katika michezo ya Paralimpiki

Ayatullah Khamenei amezungumzia njama za wanaolitakia mabaya taifa za kupotosha "utambulisho, ukweli na imani" ya taifa la Iran kusema: Wanadai kuwa hisia za kidini zimedhoofika nchini Iran, lakini ukweli ni kwamba, mashujaa wa Iran wanapoibusu Qur'ani na kusujudu kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu mbele ya macho ya labda mamia ya mamilioni ya watazamaji, wanakuwa wamedhihirisha ukweli na utambulisho wa taifa la Irani, kushikamana kwake na imani na juhudi za kulinyanyua juu zaidi taifa la Iran. Ameongeza kuwa, ishara kama hizo za kuvutia macho zilionekana katika utendaji wa wanariadha wa Iran. 

Katika Michezo ya Olimpiki ya Walemavu ya Paris, Iran ilishika nafasi ya 14 ikiwa na jumla ya medali 25, zikiwemo 8 za dhahabu, 10 za fedha na 7 za shaba.