Sep 18, 2024 12:03 UTC
  • Timu ya madaktari ya Iran yawasili Lebanon kusaidia wahanga wa hujuma ya kigaidi ya Israel

Timu ya misaada ya kimatibabu ya Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran (IRCS) imewasili Lebanon kusaidia wahanga wa shambulio baya la kigaidi la utawala wa Israel katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Mkuu wa IRCS, Pirhossein Kolivand, pamoja na timu ya kutoa misaada inayojumuisha madaktari 12, wauguzi 12 na wahudumu wa afya, imewasili Lebanon leo Jumatano, kusaidia mchakato wa matibabu ya waliojeruhiwa katika hujuma ya kigaidi ya Israel.

Kolivand amesema, idadi kubwa ya watu waliojeruhiwa ambao wanahitaji huduma kubwa zaidi za matibabu na afya watahamishiwa katika mji mkuu wa Iran, Tehran.

Amesema kuwa uamuzi wa kutuma timu ya madaktari nchini Lebanon ulichukuliwa baada ya mkutano wa dharura wa IRCS kuhusu tukio hilo.

Watu 12 waliuawa na wengine 3,000 kujeruhiwa jana Jumanne nchini Lebanon baada ya vifaa vya mawasiliano visivyo na waya, vinavyojulikana kama pager, kulipuka katika maeneo tofauti nchini Lebanon.

Beirut, Lebanon

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa, milipuko hiyo imesababishwa na shambulio lililoratibiwa na utawala wa Israel.

Kufuatia shambulio hilo la kigaidi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi alisema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kutoa msaada wowote unaohitajika kwa ajili ya matibabu ya majeruhi au kuhamishiwa Tehran kwa ajili ya matibabu.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, baada ya kushindwa kijeshi, utawala ghasibu wa Israel sasa unatumia mashambulizi ya kigaidi dhidi ya watu wa kawaida wa Lebanon na Gaza, jambo ambalo litaharakisha kuangamia kwake.