Araghchi: Tumejiandaa kwa mashambulio tarajio ya Israel, jibu letu litakalofuata litakuwa kali zaidi
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, operesheni ya makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni wa Israel yalikuwa ni ya kujihami kikamilifu na kusisitiza kuwa: Iwapo utawala wa Kizayuni utataka kujibu mashambulio hayo, basi jibu letu litakalofuata litakuwa kali zaidi.
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo pambizoni mwa kikao cha baraza la mawaziri na kulitaja shambulio kali la makombora la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya utawala katili wa Israel kuwa limeendana na haki ya halali ya kujilinda kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha hati ya Umoja wa Mataifa.
Aidha Araghchi amesema: Picha zinazohusiana na operesheni ya Ahadi ya Kweli-2 ziko wazi kabisa kwamba tumefikia malengo yetu na shabaha yetu ilikuwa ni kulenga maeneo ya kijeshi na hatukushambulia maeneo yoyote ya raia na hii ni moja ya kanuni na maadili yetu tofauti na utawala wa Kizayuni ambao umelifanya kuwa ada na mazoea suala la kushambulia miji na watu wasio na hatia.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) jana Jumanne usiku Oktoba Mosi lilitoa taarifa na kutangaza kuwa: katika kutoa jibu kwa hatua ya kuwaua shahidi Mujahid Ismail Hania, Sayyid Hassan Nasrullah na Abbas Nilfourusha Mkuu wa operesheni za IRGC imezilenga ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).
Kwa mujibu wa tangazo la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, asilimia 90 ya makombora hayo yalifanikiwa kulenga shabaha zilizokusudiwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.