Sisitizo la Iran la kufikiwa makubaliano ya nyuklia ya haki na yenye uwiano
(last modified Sat, 03 May 2025 10:59:22 GMT )
May 03, 2025 10:59 UTC
  • Sayyid Abbas Araqchi
    Sayyid Abbas Araqchi

Kufuatia kuakhirishwa duru ya nne ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani, Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, Tehran imeazimia kufikia makubaliano ya haki na yenye mlingano kuliko wakati mwingine wowote.

Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yalianza Aprili 12 mwaka huu. Duru za pili na tatu za mazungumzo hayo zilifanyika tarehe 19 na 26 mwezi huo wa Aprili. Ilitazamiwa kuwa duru ya nne ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili ingefanyika leo Jumamosi lakini Badr bin Hamad  al Busaidi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, ametangaza kuwa: "Duru ya nne ya mazungumzo ya Iran na Marekani imesogezwa mbele hadi tarehe nyingine kutokana na matatizo ya kilojistiki." 

Tarehe mpya za mazungumzo hayo itatangazwa baada ya makubaliano kati ya pande zote. Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman na Sayyid Abbas Araqchi wamesema kuwa sababu ya kuakhirishwa mazungumzo hayo ni matatizo ya kilojistiki na kiufundi, lakini upande wa Marekani hadi sasa haujatoa maoni yoyote kuhusu suala hilo. 

Pamoja na hayo, Marco Rubio, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amedai kuwa ikiwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka tu nishati ya nyuklia kwa jili ya matumizi ya amani haina haki ya kurutubisha urani na itapasa kuagiza madini hayo kutoka nje. 

Marco Rubio 

Matamshi haya yanadhihirisha mkinzano wa wazi kati ya viongozi wa serikali ya Trump kuhusu mazungumzo ya nyuklia na Iran. Hadi kufikia sasa, Witkoff ambaye anaongoza ujumbe wa Marekani katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Iran hajasema kwamba  Iran haina haki ya kurutubisha urani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kufanya duru tatu za mazungumzo ametangaza kuwa upande wa Marekani hadi sasa haujawasilisha takwa lolote lisilo la kimantiki. Nukta nyingine ni kwamba, sambamba na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, serikali ya Washington mara kadhaa imeiwekea Iran vikwazo vipya.

Vikwazo vya hivi karibuni zaidi viliwekwa na serikali ya Marekani siku ya Jumatano iliyopita. Kuwekwa vikwazo hivyo vipya sambamba na mazungumzo yanayofanyika sasa baina ya pande mbili ni kielelezo cha wazi cha kuendelea misimamo ya kiuhasama ya serikali ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu katika kalibu ya sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu.

Esmail Baqaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran juzi Alkhamisi aliashiria siasa za kiuhasama, zilizo kinyume cha sheria na dhidi ya ubinadamu za Marekani dhidi ya wananchi wa Iran na kuvitaja vikwazo vya kidhalimu vya nchi hiyo kuwa ni kinyume na misingi na kanuni za haki za kimataifa ikiwemo misingi ya haki za binadamu. Baqaei ametahadharisha kuwa Marekani ndio itakayobeba dhima ya matokeo ya hatua zake kinzani.

Esmaill Baqaei 

Licha ya kuendelea misimamo ya kiuadui na inayokinzana ya viongozi wa Marekani kuhusiana na mazungumzo ya nyuklia, Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: "Kwa upande wa Iran, hakuna mabadiliko yoyote katika azma yetu ya kufikia suluhu ya mazungumzo. Tumedhamiria pakubwa kuliko wakati mwingine wowote kufikia makubaliano ya haki na yenye uwiano; Makubaliano ambayo yatahakikisha vikwazo vinakomeshwa na kujenga hali ya kuaminiana ya kwamba miradi ya nyuklia ya Iran itaendelea kuwa ya amani siku zote kwa sharti makubaliano hayo yatoe dhamana ya kuheshimiwa kikamilifu haki za Iran." 

Msimamo na kauli hii ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, zaidi ya kitu kingine chochote, inadhihirisha azma ya Tehran ya kulinda maslahi yake ya kitaifa dhidi ya mashinikizo ya kimataifa hususan mashinikizo ya Marekani. Kwa upande mmoja, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasalimi amri mbele ya mashinikizo, na kwa upande mwingine, itafanya juhudi za kuhakikisha kuwa haki zake kamili za nyuklia zinaheshimiwa. 

Nukta ya mwisho ni kuwa, Marekani na nchi za Ulaya zinapasa kutilia maanani ukweli kwamba, mashinikizo yoyote au vikwazo vipya vinaweza kuondoa hali ya kuaminiana. Kwa msingi huo, kuna udharura wa kuwepo anga chanya na kuaminiana kwa ajili ya mazungumzo.