Mauzo ya tende za Iran nje ya nchi yapindukia dola milioni 205 kwa mwaka
Iran iliuza tende zenye thamani ya zaidi ya dola milioni 205 katika mwaka wa kalenda wa Kiirani wa 1403 (uliomalizika Machi 20, 2025), kwa mujibu wa taarifa mpya kutoka Mamlaka ya Forodha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRICA), ikionyesha nafasi imara ya nchi hii katika soko la kimataifa la tende.
Iran ni mzalishaji wa pili wa tende duniani baada ya Misri, ikizalisha takribani tani milioni 1.4 za tende kila mwaka kutoka kwenye hekta 300,000 za mashamba. Ingawa Misri inaongoza kwa uzalishaji wa jumla, Iran inaongoza kwa utofauti wa aina za tende, na hivyo kuvutia watumiaji wa ladha mbalimbali za tende duniani.
Soko la ndani hutumia karibu asilimia 70 ya tende zinazozalishwa, ambapo asilimia 40 ya matumizi hayo hufanyika katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Mikoa mikuu ya uzalishaji wa tende nchini Iran ni pamoja na Sistan-Baluchestan, Hormozgan, Khuzestan, Bushehr, Fars, na Kerman, ambayo ina hali ya hewa na mazingira bora kwa kilimo cha tende.
Ufanisi wa mauzo ya tende nje ya nchi ni sehemu ya mwelekeo mpana wa ukuaji wa biashara ya kilimo ya Iran. Mamlaka ya Forodha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeripoti kuwa mauzo ya bidhaa za kilimo nje ya nchi yaliongezeka kwa asilimia 29 mwaka jana, na kufikia dola bilioni 5.2. Kwa uzito, Iran ilisafirisha tani milioni 7.6 za bidhaa za kilimo likiwa ni ongezeko la asilimia 11 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.
Bidhaa zenye thamani kubwa kama pistachio, nyanya na tende ndizo zinazoongoza katika sekta ya kilimo. Pistachio bado ndilo zao kuu linaloingiza fedha nyingi zaidi, kwa mapato ya dola bilioni 1.5, ikifuatiwa na nyanya kwa dola milioni 233 na tende dola milioni 205.
Kadri Iran inavyotafuta kupanua msingi wake wa mauzo ya nje yasiyotegemea mafuta, utendaji thabiti wa sekta ya kilimo, hasa mazao yenye faida kubwa kama tende, unatoa fursa ya mkakati wa kuongeza mauzo ya nje na kukuza maendeleo ya kiuchumi vijijini.