Ujumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran katika kufafanua upya diplomasia ya kikanda
(last modified Tue, 20 May 2025 13:01:21 GMT )
May 20, 2025 13:01 UTC
  • Ujumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran katika kufafanua upya diplomasia ya kikanda

Kikao cha nne cha Jukwaa la Mazungumzo Ya Tehran kimefanyika hapa mjini Tehran, kikisisitiza "wakala wa kikanda" na ulazima wa kuunda utaratibu mpya kutoka ndani ya eneo.

Mkutano huo ulifanyika Jumapili na jana Jumatatu, Mei 18 na 19, 2025 ukiongozwa na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Sayyid Abbas Araghchi. Wageni 200 kutoka nchi 53 duniani wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu wa nchi mbalimbali pia walishiriki katika mkutano huo.  Miongoni mwa walioshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran ni wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, jumbe kutoka nchi za Amerika ya Kaskazini, Umoja wa Ulaya, Uingereza, Uturuki, Armenia, India, Japan, China, Russia, Saudi Arabia, Iraq na nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni na wawakilishi maalumu wa serikali.

Wakati ambapo mfumo wa kimataifa unakabiliwa na changamoto kubwa, Iran inajaribu kukuza mazungumzo mapya kwa kuwakaribisha watendaji wa kikanda ambao wanasisitiza "maelewano" na "kujitegemea kikanda." Mbinu hii inaweza kuleta mabadiliko katika mahusiano ya kimataifa katika eneo la Asia Magharibi au kutoa changamoto kwa milinganyo ya jadi ya nguvu. Badala ya kuangazia kwa kina migogoro ya sasa, mkutano umesisitiza juu ya kujenga simulizi za ndani na diplomasia ya ushirikiano.

 

Hali ya sasa ya  Palestina, Muqawama, matukio yanayoendelea kushuhudiwa sasa, mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, utaratibu mpya wa eneo la Asia Magharibi na miundo mbadala ya mfumo wa kimataifa ni mada zilizojadiliwa na kuchunguzwa katika Mkutano wa Kimataifa wa Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran.

Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa pia ni makubaliano badala ya makabiliano. Kutiliwa mkazo katika mazungumzo ya mpakani na ushirikiano wa pande nyingi, kwa lengo la kupunguza mivutano ya kihistoria.

Kongamano la Kimataifa la Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran ni tukio la kidiplomasia na kiutamaduni ambalo linalenga kuimarisha mazungumzo kati ya nchi na staarabu mbalimbali hususan katika Mashariki ya Kati na Ulimwengu wa Kiislamu. Jukwaa hili pia linatumika kama sehemu ya kubadilishana mawazo kati ya nchi na tamaduni mbalimbali, na huchukua hatua za kupunguza mivutano na kuzidisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatumia mkutano huu kueleza misimamo yake katika nyanja za kisiasa, kiusalama na kiutamaduni, na kuwasilisha maoni na vipaumbele vyake katika uga wa siasa za nje kuhusu masuala ya kimataifa. Moja ya mada kuu za mkutano huu ni kutilia mkazo mshikamano wa Ulimwengu wa Kiislamu katika kukabiliana na changamoto kama vile misimamo mikali, vikwazo na uingiliaji kati wa mataifa ajinabi.

Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran akihutubia katika Kongamano la Kimataifa la Jukwaa la Mazungumzo ya Tehran

 

Akizungumza katika kongamano hilo, Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alisisitiza kwamba, mustakabali wa Mashariki ya Kati unapaswa kubuniwa katika "miji mikuu ya eneo" na sio katika vituo vya nguvu za ulimwengu.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, Iran inajaribu kuwasilisha ramani mpya ya njia ya ushirikiano wa kikanda kwa kufafanua upya dhana muhimu kama vile "uhuru" na "mtangamano."

Mintarafu hiyo tunaweza kusema kuwa, Kongamano la Mazungumzo ya Tehran sio tu kwamba ni mkutano wa kidiplomasia, bali ni zaidi ya hilo kwani unaonyesha juhudi za Iran za kufafanua jukumu lake kama "mbunifu wa ushirikiano wa kikanda."