Iran kuzindua taasisi mpya za kurutubisha urani. Ni jibu kwa hatua ya IAEA
Wizara ya Mambo ya Nje na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran zimetoa taarifa ya pamoja kujibu hatua ya kisiasa ya nchi za Magharibi katika Bodi ya Magavana ya IAEA dhidi ya mradi wa amani wa nyuklia wa Iran na kusema kuwa itazindua taasisi mpya za kurutubisha urani.
Katika taarifa ya pamoja, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Shirika la Nishati ya Atomiki zimelaani hatua ya Marekani na nchi tatu za Ulaya (Ujerumani, Uingereza na Ufaransa) ya kupitisha azimio katika Bodi ya Magavana ya IAEA na kuitaja hatua hiyo kuwa ni kulitumia vibaya baraza hilo kisiasa na bila ya kuzingatia sheria wala kuchukua maamuzi ya kiufundi.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitekeleza wajibu wake wa kulinda usalama, na hadi sasa hakuna ripoti yoyote ya IAEA iliyoweza kutolewa kuthibitisha kuwa Iran imekwenda kinyume na ahadi zake za matumizi ya amani ya nishati hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: Tunaichukulia ripoti ya IAEA kuwa ya kisiasa na ya upendeleo kabisa, nchi hizi nne zimeenda mbali zaidi na kuandaa azimio ambalo hata vifungu vyake vikuu vinakinzana na ripoti ya kisiasa ya Mkurugenzi wake Mkuu. Kwa kuwa nchi hizi zinafuata malengo yao ya kisiasa na zimeshindwa kugundua jambo lolote tata katika shughuli za hivi sasa za nyuklia za Iran; zimekimbilia madai yanayohusiana na kipindi cha zaidi ya miaka 25 iliyopita ambayo yalishapatiwa ufumbuzi kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Iran imetangaza kuwa amri zinazohitajika zimetolewa na mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki ili kuzindua kituo kipya cha kurutubisha urani katika eneo salama na kubadilisha mashine za kizazi cha kwanza katika Kituo cha Fordow na kuzifanya za kisasa kabisa. Hatua nyingine pia zinapangwa kuchukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kujibu hatua hiyo ya kisiasa ya IAEA na zitatangazwa baadaye.