Iran yaitisha kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia mashambulizi ya Israel
(last modified Fri, 13 Jun 2025 08:10:08 GMT )
Jun 13, 2025 08:10 UTC
  • Iran yaitisha kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia mashambulizi ya Israel

Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewasilisha ombi rasmi kwa Umoja wa Mataifa ikiitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama, kufuatia kile ilichokiita “kitendo cha wazi cha uchokozi” kilichotekelezwa na Israel dhidi ya ardhi ya Iran.

Kupitia barua iliyowasilishwa na Ujumbe wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Tehran imelaani mashambulizi hayo ya angani na kuitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua ya haraka kulaani na kushughulikia ukiukaji huo wa mamlaka ya taifa huru.

“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajibu vitendo hivi vya kigaidi na vya kuvunja sheria kwa njia ya maamuzi, kwa kiwango kinachonasibiana, na kwa namna ya kuzuia marudio yake – kwa wakati na mahali tutakapochagua,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.

Iran imesisitiza kuwa kutetea mipaka ya nchi, usalama wa taifa na raia wake ni haki ya msingi na isiyoweza kujadiliwa.

“Utawala wa Kizayuni utalipia gharama kubwa kwa uchokozi huu na kwa makosa yake ya kimkakati,” taarifa hiyo imesisitiza.

Katika barua rasmi na ya dharura iliyowasilishwa kwa Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Balozi Amir Saeed Iravani, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, amelaani vikali mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni kwa msaada wa Marekani dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya amani na viongozi waandamizi wa kijeshi wa Iran.

Katika barua hiyo, Iran imeitaka jumuiya ya kimataifa kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama na kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo vya kihalifu na vya kichokozi vya Israel.

Barua hiyo imeeleza kuwa: “Utawala wa Kizayuni umefanya mashambulizi ya kijeshi yaliyoratibiwa na yenye nia mbovu dhidi ya vituo vya nyuklia na miundombinu ya kiraia ya Iran, jambo ambalo ni ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na misingi ya sheria za kimataifa. Mashambulizi haya yanatishia kwa kiwango kikubwa amani na usalama wa kieneo na wa kimataifa.”

Iravani amefichua  kuwa kituo cha nyuklia cha Natanz, ambacho kipo chini ya usimamizi kamili wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), kilikuwa miongoni mwa malengo ya mashambulizi hayo. Barua hiyo imeendelea kueleza kuwa: “Shambulizi la makusudi dhidi ya kituo cha nyuklia kinachodhibitiwa na IAEA si tu linahatarisha maisha ya raia wa kawaida, bali pia linaweza kusababisha janga la mionzi lisiloweza kurekebishwa katika eneo lote. Ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Kimataifa wa Kulinda Usalama wa Nyenzo za Nyuklia na makubaliano ya kisheria chini ya mfumo wa ufuatiliaji wa nyuklia.”

Iran imeonya kuwa mashambulizi hayo yanahatarisha msingi mzima wa utawala wa kimataifa wa kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, na yanadhoofisha hadhi na mamlaka ya IAEA.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa endapo vitendo hivyo vitapita bila kuchukuliwa hatua, vinaweza kuwa kielelezo hatari kwa mataifa mengine, na hivyo kuhatarisha usalama wa pamoja wa dunia.

Katika sehemu nyingine ya barua hiyo, Iran imesema kuwa mashambulizi hayo yamehusisha operesheni za wazi za ugaidi ndani ya mji mkuu wa Iran, ambapo zimepelekea kuuawa kwa makamanda waandamizi wa kijeshi na wanasayansi wakuu wa nyuklia wa taifa hili.
Mashambulizi hayo yameelezwa katika barua hiyo kama mfano wa wazi wa “ugaidi wa kiserikali”, huku Iran ikieleza kwamba:

“Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni amekiri wazi na kwa kiburi kuhusika na uhalifu huu, jambo ambalo ni ushahidi wa kukiri hadharani kufanya uhalifu wa kimataifa.”

Iran imesisitiza kuwa mashambulizi ya Israel ni uvunjaji mkubwa wa mamlaka na uhuru wa taifa huru mwanachama wa Umoja wa Mataifa, na kwa mujibu wa sheria za kimataifa na sheria za kibinadamu, ni tendo la uchokozi na uhalifu wa kivita.

“Vitendo hivi ni ukiukaji wa moja kwa moja wa Kifungu cha 2(4) cha Hati ya Umoja wa Mataifa, kinachopiga marufuku tishio au matumizi ya nguvu dhidi ya mamlaka ya nchi au uhuru wa kisiasa wa taifa lolote."

Katika taarifa yake, ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa umesema:

“Mashambulizi haya ya hivi karibuni, yaliyoratibiwa kwa uangalifu, ni tangazo la wazi la vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ni mwendelezo wa tabia hatarishi na isiyo halali ya utawala wa Kizayuni, ambao kwa hakika ni miongoni mwa tawala za kigaidi na zisizoheshimu sheria zaidi duniani.”

Katika hitimisho la barua rasmi iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, na kusisitiza kuwa Iran ina haki ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya kigeni.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa:

“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, itatoa jibu kali dhidi ya vitendo vya ukiukaji sheria na kinyama vya Israel. Jibu hilo litatolewa  kwa wakati na mahali itakapochagua, na litakuwa na lengo la kumzuia adui kutekeleza tena uhasama wake.

Wito wa Iran kwa Baraza la Usalama unakuja wakati ambapo hali ya Asia Magharibi inazidi kuwa tete, huku wachambuzi wakionya kuwa huenda hali hii ikavuruga uthabiti wa kimataifa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa.