Serikali ya Iran yaapa kulipiza kisasi baada ya hujuma ya mashambulizi ya Israel
(last modified Fri, 13 Jun 2025 08:37:50 GMT )
Jun 13, 2025 08:37 UTC
  • Serikali ya Iran yaapa kulipiza kisasi baada ya hujuma ya mashambulizi ya Israel

Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa tamko kali la kulaani mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Israel alfajiri ya leo Ijumaa, ambayo kwa mujibu wa ripoti za awali, yamepelekea kuuawa shahidi maafisa waandamizi wa kijeshi pamoja na wanasayansi mashuhuri wa nyuklia wa Iran. Tehran imetaja mashambulizi hayo kama “kitendo cha kigaidi kinachoakisi uoga.”

Kupitia taarifa rasmi, serikali ya Iran imelaumu  utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuvunja sheria za kimataifa kwa makusudi, na kujaribu kuchochea vita wazi wazi kupitia kampeni ya mauaji ya kulenga watu binafsi, ikilenga hasa kuhujumu juhudi za kidiplomasia zinazohusu mpango wake wa nyuklia.

Aidha taarifa hiyo imebaini kuwa: “Utawala wa Kizayuni umechagua njia ya ugaidi na jinai za kivita kwa kulenga ardhi, makamanda na wanasayansi wetu."

Miongoni mwa waliouawa katika mashambulizi hayo ni maafisa wa ngazi za juu katika jeshi la Iran na wanasayansi waliohusika katika miradi nyeti ya taifa hili.

Serikali ya Iran imesisitiza kuwa mashambulizi hayo ni “kitendo cha vita,” ikisisitiza kuwa japokuwa Iran haijaanzisha vita vyovyote kwa zaidi ya karne mbili, inalazimika kujibu kwa nguvu kamili pale mamlaka na heshima ya taifa inapokanyagwa.

Taarifa hiyo imeweka bayana kuwa: “Kisasi si chaguo tu, bali ni haki yetu halali, na ni jambo lisiloepukika. Tayari hatua za kijeshi, kisheria na za kidiplomasia zimeanza kuchukuliwa."

Tehran pia imezilaumu serikali za Magharibi kwa "kushiriki kwao kwa kimya" katika uhalifu huo, na kuzitaka taasisi za kimataifa, hasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuchukua hatua kwa ajili ya kulinda utawala wa sheria wa kimataifa.

Hata hivyo, serikali ya Iran imeonya kuwa haitasubiri idhini ya dunia kabla ya kuchukua hatua.

“Kisasi kiko karibu, karibu zaidi na koo za Wazayuni kuliko walivyowahi kudhani. Hili si sauti ya serikali pekee, bali ni kilio cha taifa zima.”