Operesheni ya Ahadi ya Kweli 3; Israel yakumbwa na wimbi la makombora ya Iran
(last modified Sat, 14 Jun 2025 02:51:26 GMT )
Jun 14, 2025 02:51 UTC
  • Operesheni ya Ahadi ya Kweli 3; Israel yakumbwa na wimbi la makombora ya Iran

Vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimeanza kufanya wimbi la mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel, ili kulipiza kisasi kufuatia hujuma za utawala huo wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Iran.

Awamu ya tatu ya operesheni ya kijeshi ya kulipiza kisasi ya Iran - Operesheni ya Ahadi ya Kweli 3 - ilianza mwendo wa saa saba na nusu usiku wa kuamkia leo kwa saa za hapa Iran, baada ya awamu mbili zenye mafanikio, ambapo maeneo mengi ya kimkakati ya Israel yalilengwa.

Shirika la habari la IRNA limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, Israel imeanza kuhisi ghadhabu ya Iran usiku wa kuamkia leo, wakati Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilipoanzisha wimbi la mashambulizi dhidi ya utawala huo haramu.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari vya Israel, katika wimbi hili jipya, makombora ya Iran yamepiga maeneo tofauti mjini Tel Aviv, Jerusalem (al-Quds), Ziwa Tiberias, Haifa, Beersheba na maeneo mengine.

Uharibifu mkubwa zaidi umeripotiwa Tel Aviv, ambapo angalau kombora moja lilipiga jengo la orofa 50, na kusababisha mripuko mkubwa ambao ulipelekea wingu jeusi la moshi kutanda angani. Ripoti za vyombo vya habari vya Israel zimeelezea kujiri matukio ya purukushani na wahaka huko Tel Aviv, huku huduma za dharura hasa kusini mwa mji huo zikihangaika huku na kule kuwahudumia majeruhi.

Makombora ya Iran yauteketeza mji wa Tel Aviv

Kutokana na hali nyeti ya maeneo yaliyolengwa, kikosi cha jeshi la Israel kinachojiita 'Home Front Command' kimeripotiwa kulazimisha vyombo vya habari kuzima au kuchuja baadhi ya habari ili kuepusha aibu zaidi.

Katika taarifa ya pili baadaye saa sita usiku, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC lilisema vitengo vya makombora na ndege zisizo na rubani vililenga kambi za jeshi la Israel ambazo zilitumiwa kuanzisha mashambulio dhidi ya Iran, pamoja na utengenezaji wa silaha za kiviwanda na maeneo mengine ya kijeshi ndani ya Israel.

Taarifa hiyo imesema kuwa, taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa, ikiwa ni pamoja na picha za satelaiti, zilionyesha makumi ya makombora ya balestiki ya Iran yalikuwa yamelenga shabaha zao kwa usahihi.