Mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani ya Iran dhidi ya Israel, mwisho wa zama za "kushambulia na kukimbia" kwa Israel.
(last modified Sun, 15 Jun 2025 12:15:50 GMT )
Jun 15, 2025 12:15 UTC
  • Mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani ya Iran dhidi ya Israel, mwisho wa zama za

Baada ya utawala wa Kizayuni kuishambulia Iran kwa ushirikiano wa Washington asubuhi ya Ijumaa, Juni 13, na kupelekea kuuawa shahidi idadi kubwa ya makamanda waandamizi wa kijeshi na wanasayansi, pamoja na raia wa kawaida, Iran, kama ilivyoahidi awali, ilianza kutoa jibu kali kwa jinai hiyo na mauaji ya kimbari Ijumaa usiku kupitia operesheni ya mashambulio ya makombora na ndege zisizo na rubani, iliyopewa jina la Ali ibn Abi Talib.

Kuanzia mwendo wa saa nne Ijumaa usiku, wanajeshi wa Iran walianzisha Operesheni ya "Ahadi ya Kweli 3" na kujibu vilivyo mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni kwa kurusha mamia ya makombora mbalimbali ya balistiki kuelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Katika kuashiria mashambulizi hayo, CNN ilinukuu jeshi la Israel likisema: "Israel yote iko chini ya moto wa Iran unaoendelea kuwaka." Mkutano wa waandishi wa habari na msemaji wa jeshi la Israel pia ulikatizwa ghafla kufuatia kuanza kwa operesheni hiyo. Vyombo vya habari vya Kiibrania viliripoti kuwa moto ulikuwa ukiongezeka karibu na Al-Kiryah, makao makuu ya Wizara ya Vita huko Tel Aviv. Wimbi la pili la mashambulio hayo lilianza karibu saa tano usiku.

Ilikuwa karibu saa nane usiku wa manane wakati vyombo vya habari vya Israel viliripoti wimbi la tatu la mashambulizi ya makombora ya Iran kwenye maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Katika shambulio hilo, idadi kubwa ya makombora ya Iran yalipenya kirahisi kwenye ulinzi wa anga wa Israel na kulenga shabaha zilizoainishwa katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Vyanzo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa takriban makombora 150 yalirushwa katika wimbi hilo jipya.

Al-Mayadeen ilitangaza kuwa wimbi la nne la mashambulio ya makombora ya Iran katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu lilianza saa tano asubuhi. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kiebrania, makombora ya Iran yalipiga Tel Aviv, Jerusalem, Haifa, Beersheba, Bahira na Galilaya, ambapo sauti za ving'ora zilisikika kutokea kaskazini kuelekea kusini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel). Wengi wamesema kuwa mashambulio kama hayo hayajawahi kuonekana tena katika historia ya utawala huo haramu. 

Mashambulio ya Iran Tel Aviv

Majira ya saa 12 na nusu asubuhi vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuanza kwa wimbi la tano la mashambulizi ya makombora ya Iran, vikisema kuwa wimbi la tano la makombora ya Iran lililenga maeneo yote ya Israel. Viliripoti kuwa, wimbi hilo la makombora lililenga maeneo ya Tiberias, Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Galilaya ya Chini.

Ripoti za awali zinaonyesha kuwa makumi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran zilifanikiwa kupenya matabaka mengi ya ulinzi wa anga ya Israel na kupiga maeneo mengi nyeti. Baadhi ya ripoti zinaonyesha kuwa makombora ya Iran yalipiga Tel Aviv, Netanya, Herzliya, Haifa, Tamra, Ashdod na Kerioth, na kusababisha moto mkubwa.

Katika mawimbi hayo, makombora ya Iran yamefanikiwa kupenya na kupiga moja ya miundombinu muhimu zaidi ya kudhamini mafuta ya utawala wa Israel huko Haifa, ambayo huzalisha 40% ya petroli na 60% ya dizeli kwa matumizi ya utawala huo. Zaidi ya hayo, makombora ya Iran yamelenga na kugonga vituo muhimu vya kistratijia vya Israel vikiwemo vya kusambaza nguvu za umeme, jambo ambalo limeibua matatizo makubwa katika sekta hiyo.

Vyombo vya habari vya Kiibrania vimesema kuwa hayo ni mashambulizi makali zaidi ya moja kwa moja ndani ya utawala wa Kizayuni. Gazeti la Kizayuni la “Ma’ariv” limeandika: “Kwa sasa tuko chini ya mashambulizi makali zaidi ambayo hayajawahi kutokea tena katika historia ya Israel; yuko wapi Waziri Mkuu Netanyahu?!”

Afisa mmoja wa ngazi za juu katika masuala ya usalama wa Iran ameiambia Al Jazeera kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiandaa kwa ajili ya makabiliano ya muda mrefu na kwamba itaongeza kiwango cha mashambulizi yake ikiwa uchokozi wa Wazayuni utaendelea. Amesema: "Tehran haikuanzisha vita, lakini ni sisi tutakaoamua uchokozi huu utamalizika lini." 

Utawala wa Kizayuni ukiwa ni utawala ghasibu na wa kichokozi daima umekuwa ukichochea na kuzishambulia nchi jirani za eneo hili bila kujali lolote. Baada ya kuanza Vita vya Gaza mwanzoni mwa Oktoba 2023, Israel, sambamba na kuendesha mauaji ya umati dhidi ya wakazi wa ukanda huo na ambayo yamepelekea kuuawa zaidi ya raia 55,000 wasio na hatia, baadaye ilianzisha mashambulio ya anga na ya nchi kavu dhidi ya Lebanon, na kisha Syria, baada ya kuanguka kwa serikali Bashar al-Assad. Baadaye utawala wa Kizayuni katika kukabiliana na hatua za muqawama wa Yemen za kuunga mkono wakaazi wa Gaza, ulianzisha mashambulizi makali ya anga dhidi ya nchi hiyo kwa lengo la kuharibu miundombinu yake. Utawala huu pia umeshambulia vituo vya muqawama wa Iraq. Kwa hivyo, ni wazi kwamba Israeli kimsingi ni utawala wa kichokozi unaochochea vita, ambapo eneo la Asia Magharibi halijashuhudia amani tangu kuasisiwa kwake kinyume cha sheria mnamo Mei 1948.

Israel haina uwezo wa kuendeleza vita

Nukta muhimu ni kwamba, utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono usio na kikomo wa Marekani, daima umekuwa ukichokoza na kuzishambulia nchi za eneo bila kuogopa lolote. Pamoaj na hayo lakini sasa Israel katika kueneza chokochoko zake mpya za kijeshi dhidi ya Iran, inakabiliwa na hali mpya na ambayo haijawahi kushuhudiwa tena katika historia yake. Majibu makali na ya kuumiza ya kijeshi ya Iran kwa hatua ya jinai ya Israel yameibua hofu kubwa miongoni mwa Wazayuni wanaoishi katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuvuruga pakubwa mwenendo wa kawaida wa maisha wa Israel. Tel Aviv inajua kwa hakika kwamba kwa kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya Iran, itakabiliwa na jibu kali na la kuumiza zaidi kutoka Iran, jibu ambalo bila shaka litatikisa misingi ya utawala huo wa Kizayuni. Israel na Marekani, zikiwa washirika wa kistratejia zinapasa kufahamu kwamba zama za kushambulia na kisha kukimbia zimekwisha, na hatua yoyote ya kibabe dhidi ya Iran itakabiliwa na jibu kali na zito, jibu ambalo litatikisa misingi ya utawala huo haramu na wa jinai.