Rais Pezeshkian: Jinai za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni ni ushahidi wa uadui wake
(last modified Sun, 15 Jun 2025 12:34:04 GMT )
Jun 15, 2025 12:34 UTC
  • Rais Pezeshkian: Jinai za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni ni ushahidi wa uadui wake

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, jinai za hivi karibuni za jeshi la Kizayuni ni ushahidi wa uchokozi na upuuzaji wake wa maisha ya binadamu.

Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo leo katika mazungumzo yakke kwa njia ya somuu na Amir wa Qatar na kusema: "Wamarekani wanaunga mkono mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran na wanaamini kuwa wanaweza kutuwekea matakwa yao kwa mashinikizo."

Rais Pezeshkian ameelezea kufurahishwa kwake na kuwa pamoja uungaji mkono wa Amir wa Qatar kwa serikali na wananchi wa Iran na kusema: "Mmeona kwamba, tangu siku ya kwanza nimekuwa nikijaribu kuimarisha ushirikiano na nchi jirani na za Kiislamu kwa lengo la ukuaji na ubora wa eneo, lakini tangu siku ya kwanza utawala wa Kizayuni umekuwa ukitaka kuvuruga mchakato huu na kuzusha machafuko katika eneo hili."

Ameongeza kuwa: Ijapokuwa Wamarekani wamekuwa wakisisitiza kila mara kwamba, utawala wa Kizayuni hautachukua hatua yoyote dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila ya idhini na uratibu wao, lakini leo hii kwa bahati mbaya wanaunga mkono mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran na wanaamini kwamba wanaweza kutuwekea matakwa yao kwa mashinikizo. Amesisitiza kuwa jinai za hivi karibuni za utawala wa Kizayuni ni ushahidi wa uvamizi na upuuzaji wa utawala huo kwa maisha ya binadamu.

Rais Pezeshkian amebainisha kuwa, nina hakika kwamba uungaji mkono na uratibu wa nchi za Kiislamu utakomesha utawala huo na kukomesha uchokozi wake, hasa dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Gaza. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo wa kujilinda na haitasita kukabiliana na uchokozi dhidi ya ardhi yake na haki za watu wake.

Kwa upande wake, Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al Thani ametoa salamu zake za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Iran na kusema: "Qatar inalaani vikali hujuma hiyo ya woga na inaamini kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki kamili ya kujibu." Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani ameashiria kuwa Qatar inasimama na ndugu zake nchini Iran na inaunga mkono kanuni ya maingiliano na mazungumzo ili kutatua tofauti na kudumisha amani.