Yajue makombora ya 'Emad', 'Ghadr', na 'Kheibar Shekan' yanayotumiwa na Iran dhidi ya Israel
-
Kombora la \'Kheibar Shekan\'
Kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya Iran, kitengo cha anga za juu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kilitumia mifumo mbalimbali ya kisasa ya makombora wakati hujuma ya ulipizaji kisasi dhidi ya Israel iliyopewa jina 'Operesheni Ahadi ya Kweli III' Jumamosi.
Kwa mujibu wa Press TV, makombora ya Emad, Ghadr, na Kheibar Shekan yalitumika katika mashambulizi ya hivi karibuni yaliyolenga miji ngome za utawala wa Kizayuni wa Israel katika miji inayokaliwa kwa mabavu ya Haifa na Tel Aviv.
Kombora la 'Emad': Usahihi wa Hali ya Juu
Kombora la masafa marefu la Emad, ambalo ni toleo lililoboreshwa la Ghadr, lina mfumo wenye usahihi ulioimarishwa wa kulenga shabaha. Lilifanyiwa majaribio na kuanza kutumika mwishoni mwa mwaka 2015. Kwa mujibu wa maafisa wa jeshi la Iran, Emad lina uwezo wa kuongozwa kwa mbali hadi kufikia kenye shabaha, na hivyo kulifanya kuwa kombora la kwanza la Iran linaloongozwa kwa usahihi wa hali ya juu.
Kombora la Emad ambalo hutumia mafuta ya kioevu na lina urefu wa mita 15.5, uzito wa kilogramu 1,750, na lina kuweza kuruka masafa ya kilomita 1,700, na linajivunia na duara la uwezekano wa kosa (CEP) ni la mita 50. Hii inaashiria uwezo wa kiufundi wa hali ya juu katika kuhakikisha shabaha inafikiwa.
Kombora la 'Ghadr': Maboresho ya Nguvu na Masafa Marefu
Kombora la Ghadr, lilizinduliwa mwaka 2005, na ni toleo lililoboreshwa la kombora la masafa ya kati la Shahab-3, ambalo limekuwa likitumika nchini Iran tangu mwaka 2003. Hili ni kombora la hatua mbili, likiwa na hatua ya kwanza inayoendeshwa na mafuta ya kioevu na hatua ya pili inayoendeshwa na mafuta mango. Kuna aina tatu za kombora la Ghadr: Ghadr-S lenye masafa ya kilomita 1,350, Ghadr-H lenye kilomita 1,650, na Ghadr-F lenye kilomita 1,950.
Likiwa na urefu kati ya mita 15.86 na 16.58 na kipenyo cha kiunzi cha anga cha mita 1.25, Ghadr lina uzito kati ya tani 15 na 17.5. Kuongezeka kwa urefu wake ikilinganishwa na Shahab-3 kunaliwezesha kusheheni matangi makubwa ya mafuta na vioksidishaji, likibeba kilogramu za ziada 1,300 hadi 1,500 za propellant na kuwezesha injini kuwaka kwa sekunde kumi au zaidi za ziada. Ili kukabiliana na uzito huu ulioongezeka, kiunzi cha anga cha kombora kimejengwa kwa kutumia aloi nyepesi za alumini, kupunguza uzito wake kwa takriban kilogramu 600 ikilinganishwa na muundo wote wa chuma.

Uzito wa kichwa cha vita ulipunguzwa kutoka kilogramu 1,000 hadi 650, na kupanua masafa ya kombora kutoka kilomita 1,200 hadi karibu kilomita 2,000. Ghadr pia linajivunia muundo wa kichwa cha vita kilichobadilishwa na kuwa na umbo la "chupa ya mtoto" ambayo inaboresha aerodynamiki na usahihi. Pamoja na mfumo wa hali ya juu wa uongozi, muundo huu unapunguza duara la uwezekano wa kosa (CEP) yake kutoka mita 2,500 hadi kati ya mita 100 na 300. Hii inaashiria maendeleo makubwa katika uwezo wa kulenga shabaha.
Kombora la 'Kheibar Shekan': Uwezo wa Mashambulizi ya Kimkakati
Kombora la Kheibar Shekan ni kombora la masafa ya kati lililoundwa kwa mashambulizi ya kimkakati na limeonyesha ufanisi katika mapigano ya awali. Matoleo ya Kheibar Shekan-1 na Kheibar Shekan-2 yanasemekana kuwa na uwezo wa kupenya mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga ya Israel, ikiwemo Arrow-3 na David’s Sling. Uwezo huu ni wa kutisha kwa adui yeyote anayetegemea mifumo hiyo ya ulinzi.
Likiwa na masafa ya kukadiria ya takriban kilomita 1,450 (takriban maili 900), Kheibar Shekan linaweza kubeba kichwa cha vita cha kawaida au kisicho cha kawaida, na kulifanya kuwa hatari sana. Linatumia teknolojia ya hali ya juu ya uongozi, ikiwemo mfumo wa kubadilisha mkondo wakati wa kutua (MaRVs) ulioundwa kukwepa mifumo ya ulinzi wa makombora. Kombora hili linaendeshwa na injini ya hatua mbili ya mafuta mango, inayowezesha utayari wa kurusha haraka ikilinganishwa na makombora yanayoendeshwa na mafuta ya kioevu.
Linalenga kushambulia shabaha za kimkakati kwa usahihi, kama vile miundombinu muhimu na kambi za kijeshi ndani kabisa ya eneo la adui.

Makombora hayo matatu yenye uwezo mkubwa ni sehemu tu ya makumi ya aina ya makombora ya Iran. Majeshi ya Iran yamesisitiza kuwa uvamizi wa utawala wa Israel ukiendelea, basi makombora yenye uwezo mkubwa zaidi yatatumika.
Wimbi la hivi karibuni la mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya utawala wa Kizayuni lilianza Jumamosi usiku, kufuatia awamu ya awali ya operesheni ya kulipiza kisasi iliyozinduliwa Ijumaa. Operesheni hii ni jibu kwa mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi ya Israel katika miji tofauti ya Iran, ikiwemo Tehran Ijumaa asubuhi na vile vile Jumamosi, na kusababisha kuuawa kwa makamanda wengi waandamizi wa jeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia, wakiwemo watoto.
Operesheni hii ya kijeshi isiyo na mfano inafanywa chini ya jina la "Ya Ali ibn Abi Talib," ikiambatana na hafla ya Eid al-Ghadir. Idara ya Mahusiano ya Umma ya IRGC ilitoa taarifa ikithibitisha kuwa kitengo chake cha anga za juu kimeanzisha awamu hii mpya ya operesheni kama jibu la moja kwa moja kwa uchokozi mpya wa utawala wa Kizayuni. Baadhi ya vyombo vya habari vimeeleza shambulio la hivi karibuni la Iran kama shambulio kubwa zaidi la makombora lililowahi kufanywa na vikosi vya jeshi la Iran dhidi ya utawala dhalimu wa Israel.